BREAKING NEWS

Tuesday, September 3, 2013

SOMA HABARI YA WATOTO WA DARASA LA NNE WALIO KUNYWA GONGO

Watoto tisa wa darasa la nne wa shule ya msingi Dumbeta Wilayani Hanang’ waliokunywa gongo na kuzirai mwaka 2012 na kuzua taharuki, wamejutia kilichowatokea na kudai kuwa hawatarudia kunywa kinywaji hicho haramu.

Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi shuleni hapo, watoto hao (majina yao tunayo) walidai kuwa walikuta chupa moja inayotumika kuhifadhi maji ya lita moja na nusu ina gongo kwenye shimo la muhanga  na kuanza kunywa.

Wanafunzi hao walisema baada ya kunywa walilegea miili yao na wakaanguka chini na kuzirai kwa muda mrefu, kutokana na kunywa pombe hiyo haramu aina ya gongo iliyokuwa kwenye chupa waliyodhani kuwa ni maji ya kunywa.

Walisema walipoteza fahamu kwa takribani saa nne kutokana na
unywaji wa kinywaji hicho na waliamshwa na mwalimu wao wakiwa
wamelala kiwanjani walipokuwa wanacheza mpira wa miguu .

“Baada ya mwalimu wetu kutukosa darasani alianza kututafuta ndipo akatukuta kwenye hali hiyo na alipotuamsha akatupatia huduma ya kwanza na kisha akatupeleka hospitali kwa matibabu zaidi,” walisema.

Walisema kati yao hakuna aliyepoteza maisha na wanaendelea na shule vizuri na kuna baadhi yao wameacha shule kutokana na unywaji wa gongo, ila wamejutia kwa kukiona cha moto kutokana unywaji wa kinywaji hicho haramu.

Naye, Mkuu wa shule hiyo mwalimu Ole Langai akizungumzia masaibu hayo alisema kilichotokea kwa watoto hao kipindi kile kilikuwa hatari kwani yeye alidhani wanafunzi hao walikuwa wamekunywa sumu.

“Mimi nilidhani wale watoto watapoteza maisha  na nikijua kuwa wamekunywa sumu, kwani ningekuwa wa kwanza kuulizwa kuhusu maisha ya watoto hao ila namshukuru Mungu kwa kuwasaidia watoto hao,” alisema Langai.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates