Raisi
wa Somalia Hassan Sheikh Mohamed asema Al shabab walishirikiana na Al
Qaeda katika kushambulia jengo la kibiashara la Westgate la jijini
Nairobi
Wakati jeshi la Kenya likiarifiwa kudhibiti eneo zima la
jengo la kibiashara la Westgate jijini Nairobi,Rais wa Somalia, Hassan
sheikh Mohamud amesema kuwa wanamgambo wa Al-Shabab waliotekeleza
shambulio kwenye eneo hilo hawakufanya kazi peke yao bali walishirikiana
na kundi la Kigaidi duniani la Al-Qaeda.
Raisi wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamed akiwa mjini New York
kuhudhuria mkutano wa 68 wa Umoja wa Mataifa, amesema wanamgambo wa
Al-Shabab wameendelea kuwa kitisho cha usalama kwenye nchi yake na nchi
jirani na kwamba anatoa pole kwa wananchi wa Kenya kwa kilichotokea.
Kauli ya rais Mohamed, pia iliungwa mkono na waziri wa mambo ya
kigeni wa Kenya Amina Mohamed ambaye amesema tukio hili halikufanywa na
wanamgambo wa Al-Shabab peke yao lakini walipata usaidizi toka kwa kundi
la Al-Qaeda.
Rais wa Marekani, Barack Obama ameendelea kutoa pole kwa serikali ya
Kenya na kuahidi nchi yake kutoa ushirikiano wa kutosha kwa vyombo vya
usalama vya Kenya kudhibiti makundi ya kigaidi.
Kwa upande wake naibu wa rais wa Kenya, William Ruto ambaye alirejea
nyumbani jumatatu usiku akitokea mjini The Hague ambako anaendelea
kusikiliza kesi yake na kupewa mapumziko ya juma moja, amelaani tukio
hili na kuvipongeza vyombo vya usalama nchini humo kwa kuwadhibiti
wanamgambo hao.