HIFADHI
ZA TAIFA TANZANIA
TAARIFA KWA UMMA
KISIWA CHA SAANANE CHATANGAZWA RASMI HIFADHI YA TAIFA
Kisiwa cha Saanane
kimetangazwa rasmi kuwa Hifadhi ya Taifa kufuatia Tangazo la Serikali Namba 227 lililotolewa hivi karibuni.
Kutangazwa kwa Hifadhi ya
Taifa ya Kisiwa cha Saanane kunafuatia kupitishwa kwa Azimio la Bunge mwezi
Oktoba mwaka jana lililoridhia kupandishwa hadhi kwa kisiwa hicho kutoka Pori
la Akiba na kuwa Hifadhi ya Taifa.
Hifadhi ya Taifa ya Kisiwa
cha Saanane itakuwa na ukubwa wa kilomita za mraba 2.18 na itajumuisha maeneo
ya lililokuwa Pori la Akiba , Visiwa vya Chankende kubwa na ndogo pamoja na
eneo la maji ya Ziwa Victoria linalozunguka visiwa hivyo.
Kuanzishwa kwa Hifadhi
mpya ya Taifa ya Saanane kutawezesha haja ya kuongeza spishi mbalimbali za
wanyamapori na hivyo kuongeza utalii wa mjini, utalii wa ndani, utafiti na
kutoa elimu kwa vitendo kwa wanafunzi na wananchi watakaotembelea hifadhi hii
mpya.
Aidha, uamuzi huu
utasaidia kutunza hali ya bioanuwai, uhifadhi wa mazalia na makuzio ya samaki
na uendelezaji wa utalii wa mjini kuendelea kuimarika.
Kabla ya kupandishwa
hadhi, Kisiwa cha Saanane kilikuwa Bustani ya wanyama mwaka 1964 kabla ya
kupandishwa hadhi kuwa Pori la Akiba mwaka 1991. Ilipofika mwaka 2006, Serikali
ilikikabidhi kisiwa hicho kwa Shirika la Hifadhi za Taifa kwa ajili ya
kukiendesha na kusimamia mchakato wa kukipandisha hadhi kuwa Hifadhi ya Taifa.
Kufuatia uamuzi huu, Shirika la Hifadhi
za Taifa (TANAPA) sasa litakuwa na jumla ya Hifadhi 16 nchi nzima ambazo nyingine
ni pamoja na Serengeti; Ziwa Manyara; Tarangire na Arusha.
Nyingine ni pamoja na Kilimanjaro;
Mkomazi; Saadani; Mikumi; Milima ya Udzungwa; Ruaha; Kitulo; Katavi; Gombe;
Milima ya Mahale na Kisiwa cha Rubondo.
Wakati huohuo, eneo la Hifadhi
ya Taifa Gombe limeongezwa ukubwa kutoka Kilometa za mraba 33.74 hadi kufikia
kilometa za mraba 56. Uamuzi huu unatokana na Tangazo la Serikali Namba 228
lililotolewa hivi karibuni ambalo linafuatia Azimio la Bunge la Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania lililotolewa mwaka jana
linalohusu kuridhiwa kwa uamuzi wa kurekebisha mipaka ya Hifadhi ya
Taifa Gombe kwa kuondoa eneo la makaburi na kuliacha kwa wananchi pamoja na
kujumuisha eneo la ufukwe wa maji ya Ziwa Victoria na eneo la ukanda wa maji.
Kuongezeka kwa eneo la ufukwe wa ziwa na
ukanda wa maji kwenye eneo la hifadhi kutaongeza wigo wa shughuli za utalii
katika Hifadhi kama vile kuogelea, utalii wa boti, mitumbwi na uvuvi wa
kitalii.
Imetolewa na
Idara ya Uhusiano
Hifadhi za Taifa
Tanzania
S. L. P 3134
ARUSHA
03.09.2013