JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA UCHUKUZI
MAMLAKA YA HALI YA HEWA TANZANIA
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Taarifa hii inatoa tathmini ya mvua za masika (Machi
- Mei) 2013 na mwelekeo wa mifumo ya hali ya hewa na mvua kwa kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2013.
1.0 TATHMINI
YA MVUA KIPINDI CHA MACHI – MEI, 2013
Katika msimu uliopita wa mvua za masika 2013, maeneo
mengi ya nchi yalipata mvua za wastani
isipokuwa maeneo machache ya mikoa ya Tabora, Rukwa, Mara na Singida ambayo ilipata mvua juu ya wastani. Wakati huo
huo baadhi ya maeneo ya mikoa ya Iringa, Ruvuma, Kilimanjaro na maeneo mengi ya
mwambao wa pwani yalipata mvua chini ya
wastani.
Vifuatavyo ni viwango vya mvua pamoja na asilimia ya mvua
zilizonyesha ikilinganishwa na wastani wa muda mrefu katika baadhi ya vituo nchini:
1.1 Maeneo yanayopata misimu
miwili ya mvua kwa mwaka
Kanda ya Ziwa Victoria: Bukoba milimeta 984.9 (110.9%),
Mwanza 385.0mm (101.1%), Musoma milimeta 516.4 (127.5%), Ukiriguru milimeta 363.4
(107.5%) na Shinyanga milimeta 307.7 (61.1.0%).
Nyanda za juu kaskazini
mashariki: Arusha milimeta 368.8 (84.4%), Moshi milimeta 472.9 (77.9%), Lyamungo milimeta
655.5 (65.3%), Kilimanjaro milimeta 291.6 (95.5%) na Same milimeta 291.3 (111.8%).
Pwani ya kaskazini na
visiwa vya Unguja na Pemba: Zanzibar milimeta 534.3 (62.0%), Amani milimeta 484.0
(63.0%), Kizimbani milimeta 667.7 (75.2%), Dar es Salaam milimeta 458.8 (77.7%),
Morogoro milimeta 227.8 (55.1%), Tanga milimeta 586.7 (91.4%) na Pemba milimeta
884.0 (85.7%).
1.2 Maeneo yanayopata msimu
mmoja wa mvua kwa mwaka:
Nyanda za juu kusini magharibi: Mbeya milimeta 254.8 (85.7%),
Sumbawanga milimeta 275.0 (126.2%),
Mahenge milimeta 1215.5 (118.2%) na Tukuyu milimeta 1094.2 (96.7%).
Kanda
ya magharibi: Tabora milimeta 296.4 (135.2%), Kibondo milimeta 418.2 (94.0%) na Kigoma milimeta 318.7 (94.6%).
Pwani
ya kusini: Kilwa milimeta 346.4 (68.3%), Mtwara milimeta 404.2 (86.0%) na Naliendele milimeta 350.5 (79.4%).
Kanda
ya kati: Singida milimeta 410.0 (198.9%), Dodoma milimeta 145.1 (82.0%) na Hombolo milimeta 101.0 (52.9%).
Kanda ya kusini:
Songea milimeta 247.9 (67.5%)
Viwango vya mvua chini ya asilimia 75 ya wastani kwa
kipindi kirefu hutafsiriwa kama chini ya wastani, wakati viwango vya kati ya
asilimia 75 na 125 hutafsiriwa kama mvua za wastani na vile vya zaidi ya
asilimia 125 hutafsiriwa kama juu ya wastani.
2.0 MWELEKEO WA MVUA KIPINDI CHA OKTOBA – DISEMBA 2013
2.1 Utangulizi
Wanasayansi kutoka taasisi za hali ya
hewa kwenye nchi za Pembe ya Afrika, Afrika Mashariki ikiwemo Tanzania, na
taasisi za kikanda na kimataifa walikutana Nairobi na baaadae Eldoret, Kenya kuanzia
tarehe 12 hadi 23 Agosti, 2013 kufanya uchambuzi wa mifumo ya hali ya hewa na
kutoa mwelekeo wa mvua za msimu katika ukanda huu. Aidha, mkutano kama huo
ulifanyika pia kwa nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) huko
Harare, Zimbabwe kuanzia tarehe 19 hadi 31 Agosti, 2013 ambapo Tanzania ilishiriki. Mikutano hiyo ilikuwa inafanyika
sambamba na mkutano wa wataalam na wachambuzi wa masuala ya hali ya hewa na
klimatolojia katika Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ambapo tathmini ya kina katika mifumo ya hali ya
hewa na athari zake kwa msimu ujao wa
mvua nchini ilifanyika.Viashiria vikuu vilivyotumika ni pamoja na hali ya joto la Bahari katika maeneo ya bahari
ya Hindi, Atlantiki pamoja na yale ya tropikali ya bahari ya Pasifiki.
2.2 Mifumo ya hali ya hewa
Joto la Bahari lililopo na linalotarajiwa katika
maeneo ya tropikali ya bahari za Pasifiki, Atlantiki pamoja na Hindi lilichambuliwa.
Viashiria vingine ikiwemo mifumo na mwelekeo wa upepo ambayo huleta unyevunyevu
katika nchi yetu pia ilizingatiwa. Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba, 2013
joto la wastani hadi chini ya wastani linatarajiwa katika maeneo ya tropikali
ya bahari ya Pasifiki.
Hali ya joto la bahari inatarajiwa kuwa juu kidogo ya
wastani katika maeneo ya mashariki mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Indonesia)
katika miezi ya Oktoba hadi Novemba 2013, ikiambatana na hali ya joto la bahari
chini kidogo ya wastani katika maeneo ya magharibi mwa Bahari ya Hindi (pwani ya Afrika
Mashariki). Hali hiyo inatarajiwa
kusababisha upepo wenye unyevunyevu
hafifu kutoka bahari ya Hindi kuelekea katika maeneo mengi ya pwani ya Afrika
mashariki. Aidha, upepo kutoka magharibi katika misitu ya Kongo unatarajiwa
kuwa hafifu na hivyo kupunguza kiwango cha unyevunyevu angani katika maeneo ya magharibi
mwa nchi.
Hata hivyo, katika kipindi cha mwishoni mwa miezi Novemba hadi Desemba, 2013
kunatarajiwa kuwa na ongezeko la joto la bahari katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi hali hii
inatarajiwa kusababisha ongezeka kiasi la unyevunyevu katika maeneo ya ukanda
wa Pwani ya Afrika Mashariki.
Ongezeko kiasi la joto la bahari kusini-magharibi
mwa bahari ya Hindi katika kipindi cha Novemba na Disemba, 2013 linatarajiwa
kusababisha kuwepo kwa matukio ya vimbunga katika kipindi cha msimu wa mvua za vuli, na hivyo kuathiri mifumo ya hali
ya hewa nchini katika vipindi vifupi.
2.3 Mwelekeo wa Mvua Oktoba
- Disemba 2013 Kutokana na mwelekeo wa mifumo ya hali
ya hewa kama ilivyoelezewa hapo juu, mvua za kipindi cha Oktoba hadi Disemba,
2013 zinatarajiwa kuwa kama ifuatavyo:
(i)
Mvua za Vuli (kwa maeneo yanayopata misimu miwili ya mvua)
Msimu wa mvua wa Oktoba hadi Disemba (Vuli) ni
mahususi katika maeneo ya nyanda za juu kaskazini mashariki, pwani ya
kaskazini, kanda ya Ziwa Victoria na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma.
Mwaka huu mvua zinatarajiwa kuwa chini ya wastani
katika maeneo ya pwani ya kaskazini (mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Tanga,
kaskazini mwa mkoa wa Morogoro, pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba), nyanda
za juu kaskazini mashariki (mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara), mikoa ya Mwanza,
Simiyu na Shinyanga, maeneo ya kanda ya Ziwa Victoria (mikoa ya
Kagera, Geita na Mara), kaskazini mwa mkoa wa Kigoma pamoja na baadhi ya maeneo
ya kaskazini mwa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro yanatarajiwa kuwa na mvua za
wastani.
Kanda ya Ziwa Victoria:
(Mikoa ya Kagera, Mara, Mwanza, Geita, Simiyu na Shinyanga): Mvua zinatarajiwa kuanza katika wiki ya
pili ya mwezi Septemba, 2013 katika mkoa wa Kagera na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma
na kuendelea kusambaa katika mikoa ya Mwanza, Shinyanga, Mara, Geita na Simiyu
katika wiki ya tatu ya mwezi Oktoba, 2013. Mvua zinatarajiwa kuwa za wastani
katika maeneo ya mikoa ya Kagera, Geita, Mara na kaskazini mwa mkoa wa Kigoma. Katika
mikoa mingine ya ukanda wa Ziwa Victoria (Mwanza, Shinyanga, na Simiyu) mvua
zinatarajiwa kuwa chini ya wastani.
Ukanda wa Pwani ya Kaskazini:
(Mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Pwani, Morogoro-kaskazini pamoja na Visiwa vya
Unguja na Pemba): Mvua
zinatarajiwa kuanza wiki ya tatu ya mwezi wa Oktoba, 2013. Mvua hizo
zinatarajiwa kuwa za chini wastani katika maeneo mengi.
Nyanda za juu Kaskazini
Mashariki: (Mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara): Mvua katika maeneo haya zinatarajiwa kuanza
wiki ya nne ya mwezi Oktoba, 2013 na zinatarajiwa kuwa chini ya wastani katika
maeneo mengi ya mikoa ya Kilimanjaro, Manyara na maeneo ya kusini mwa mkoa wa
Arusha. Hata hivyo kaskazini mwa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, mvua
zinatarajiwa kuwa za wastani katika baadhi ya maeneo.
(ii) Mvua za Msimu (Novemba – Aprili) kwa maeneo
yanayopata msimu mmoja wa mvua.
Msimu wa mvua za Novemba hadi Aprili ni mahususi
katika maeneo ya magharibi mwa nchi, kati, nyanda za juu kusini-magharibi,
kusini mwa nchi na pwani ya kusini. Katika kipindi cha Oktoba hadi Disemba,
2013 maeneo mengi yanatarajiwa kupata mvua za wastani.
Kanda ya Magharibi (Mikoa ya
Kigoma, Tabora, Katavi na Rukwa):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Oktoba,
2013 katika mkoa wa Kigoma na wiki ya tatu ya mwezi Novemba, 2013 katika mikoa
ya Tabora, Rukwa na Katavi. Mvua hizi zinatarajiwa kuwa za wastani katika
maeneo ya kusini mwa mkoa wa Tabora na maeneo ya mashariki mwa mkoa wa Rukwa.
Mikoa ya Katavi, kusini mwa mkoa wa Kigoma, magharibi mwa mkoa wa Rukwa na
kaskazini mwa mkoa wa Tabora, mvua
zinatarajiwa kuwa chini ya wastani.
Kanda ya kati (Mikoa ya
Singida na Dodoma):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya pili ya mwezi
Disemba, 2013 na zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo ya kusini na
uwezekano mkubwa wa kuwa na mvua chini ya wastani katika maeneo ya kaskazini
mwa mikoa hiyo.
Nyanda za juu Kusini
Magharibi: (Mikoa ya Mbeya, Iringa, Njombe na kusini mwa Morogoro):
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Novemba,
2013 na zinatarajiwa kuwa za wastani katika maeneo mengi.
Maeneo ya kusini na pwani ya
kusini (mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara)
Mvua zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Novemba, 2013 na zinatarajiwa kuwa za wastani na upo uwezekano wa baadhi ya maeneo ya kaskazini mwa mkoa wa Lindi kuwa na mvua chini ya wastani.