Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kwenye mdahalo |
Frank Timothy Malata, mgombea Ubunge Jimbo la Mufindi Kusini.
Kwa tikeki ya Chadema akitoa maelezo.
|
Mwanafunzi Mangula akiuliza swali juu ya huduma bora ya Umeme |
Zikiwa zimebaki
siku 23 kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, hapo jana
wakazi wa Jimbo la Mufindi kusini wamewataka wagombea Ubunge na Madiwani
watakaopata nafasi ya kuwaongoza katika kipindi kinachofuata kutafuta
suluhisho la ukatili dhidi ya watoto ikiwa ni pamoja na adhabu kupita kiasi
kutoka kwa walimu na wazazi, Mimba za utotoni na kukatishwa masomo kwa
watoto kwa ajili ya ndoa ama ajira.
Hayo yalisemwa
katika mdahalo uliofanyika katika Shule ya Msingi Igowole wilayani Mufindi,
ambao ulishirikisha wanafunzi kutoka Shule za Msingi Igowole, Ibatu na
Kisalasi, pamoja na walimu, wazazi na walezi ambao waliwahoji wagombea wa
Ubunge Frank Timothy Malata (CHADEMA) pamoja na wagombea udiwani Castory
Boniface Masangula (CCM) na Israel Mpina Msalilwa (CCM).
Aidha
walisisitiza suala la upatikanaji wa viwanja vya michezo kwa watoto na
kudai kuwa michezo ni njia mojawapo ya kumbadili mtoto kimwili na
kiakili.
Akijibu hoja
kutoka kwa wananchi, Mgombea Ubunge katika Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama
cha Demokrasia na maendeleo CHADEMA Frank Timothy Malata ameahidi
kupatikana suluhisho la adha hizo na kukomesha ukatili dhidi ya watoto.
Mgombea huyo pia ameahidi kuinua michezo kwa kuanza na upatikanaji wa
viwanja bora vya michezo mbalimbali zaidi ya mpira wa
miguu.
Kwa upande wake
Mgombea Udiwani Kata ya Igowole kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi CCM
Castory Boniface Masangula ameahidi kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa
kamati za ulinzi za watoto na sekta nyingine zinazojihusisha na ulinzi wa
mtoto ili kuhakikisha watoto wanalindwa dhidi ya ukatili
wowote.
Naye Israel
Mpina Msalilwa ambae ni mgombea Udiwani wa kata hiyo kupitia CHADEMA
aliahidi kushirikiana na serikali pamoja na wadau mbalimbali kuondoa tatizo
la mrundikano wa wanafunzi madarasani pamoja na kupiga vita ukatili dhidi
ya watoto zikiwemo adhabu kupita kiasi zinazotolewa na wazazi, walezi ama
walimu.
Katika hatua
nyingine, watoto ambao ndio walengwa wakuu wa Midahalo hii walitoa maoni
yao kuwa nini kifanyike baada ya viongozi hao kushika nyadhifa wanazogombea
ambapo walitaja kuwa wanakerwa na uhaba wa vitabu, vyoo, huduma bora za
afya, umeme na usafiri na kupambana na mimba za utotoni hasa hasa kwa
wanafunzi.
Wakati huo huo,
Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Mufindi Navoneiwa Mfinanga amewataka
wagombea hao kuwa karibu na kamati za watoto ili kuhakikisha wagombea
wanatimiza ahadi zao
Midahalo hii ni
muendelezo wa midahalo ya kipindi cha redio cha Walinde Watoto
kinachoandaliwa na Kampuni ya TRUE VISION Production chini ya Wizara ya
Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto ikishirikiana na UNICEF yenye lengo la
kuibua ajenda ya watoto kuelekea Uchaguzi Mkuu 2015.
Unaweza
kusikiliza kipindi cha Walinde Watoto mahali popote kupitia redio shiriki
19 ikiwemo TBC inayorusha matangazo hayo siku ya Jumamosi kuanzia saa tisa
mchana na pia kupitia tovuti ya www.walindewatoto.org na
www.facebook.com/WalindeWatoto
“Tuwape nafasi
viongozi wanaojali watoto kwa kutetea haki zao” – Baraza la
Watoto