Wananchi wa kijiji cha Naiyobi wilaya ya Ngorongoro wakichota maji
ambayo hutumia na mifugo kijiji hicho kinakabiliwa na uhaba wa maji
Na Woinde Shizza,Arusha
Wananchi wa Kijiji cha Nayobi kilichopo tarafa ya Ngorongoro wilayani
Ngorongoro mkoani Arusha wamelalamikia kero ya uhaba wa maji
inayowasababishia kukesha kwenye bomba la kijiji kwa takribani siku tatu
wakisubiri maji jambo linalopelekea shughuli za kijamii na kiuchumi
kusimama kwa muda mrefu na kinamama kutembea umbali mrefu wakitafuta huduma
hiyo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao wamesema kuwa kwa muda mrefu
wamekua wakiteseka kupata huduma za maji huku kinamama wajawazito
wakijifungulia bombani apo baada ya kukaa kwa muda wakitafuta maji huku
wengine wakilazimika kukesha na watoto wadogo .
Wanakijiji Daniel Sereki na Rehema Laizer na wamesema kuwa kwa sasa
wanakabiliwa na tatizo kubwa la uhaba wa maji pamoja na chakula na hata
pale wanapopata chakula hukosa maji ya kupikia chakula hicho na kuziacha
familia zao zikitaabika kwa njaa.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kijiji Naiyobi Meleji Sikoni amesema kuwa
kwa muda wa miaka 20 wamekua wakikabiliwa na tatizo la uhaba wa maji hivyo
ameiomba serikali na mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro iwasaidie kutatua
tatizo hilo sugu linalowaathiri wananchi wengi.
Mgombea Ubunge Jimbo la Ngorongoro Wiliam Olenasha ameeeleza kisikitishwa
na wananchi wanaoteseka kwa kero ya maji ambayo hushirikiana na mifugo
katika matumizi yake hivyo ameaidi kutatua kero hiyo pindi atakapopata
ridhaa ya kuongoza wilaya hiyo.
Wilaya ya Ngorongoro inakabiliwa na changamoto ya uhaba wa maji pamoja na
chakula hasa katika kipindi hiki cha kiangazi ,juhudi zinahitajika kwa
upande wa serikali na Mamlaka ya Ngorongoro ili kuweza kuwanusuru wananchi
na baa la njaa pamoja na uhaba wa maji.