Septemba 30, 2015 Jijini Mbeya: Kampuni ya Tigo Tanzania kwa kushirikiana na shirika
lisilokuwa la kiserikali linalotoa misaada katika jamii lijulikanalo kama
Hassan Maajar Trust (HMT) wametoa mchango wa madawati 700 yenye thamani ya
shilingi za kitanzania milioni 49 kwenye shule za msingi
32 katika wilaya ya Rungwe, Mbozi na wilaya ya Mbeya
Mjini.
Akizungumza katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika katika moja
ya shule jijini Mbeya, Meneja Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez alisema: “
mchango huu ni sambamba na dhamira ya kampuni ya kuunga mkono mipango ya
kijamii kupitia wigo wake wa kushirikisha jamii”.
“Kupitia mchango huu, kampuni ya Tigo inawajibika katika
kutengeneza viongozi wa baadaye wakiwamo madaktari, wahandisi na wataalamu
wengine wa nchi hii, "alisema Gutierrez.
Alisema, katika miezi ya hivi karibuni kampuni ilitoa mchango kama
huo wa madawati katika mikoa ya Iringa na Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya
ahadi ya dola za Marekani 50,000 kwa serikali, ahadi ambayo kampuni ya Tigo
ilitoa mwaka jana ili kusaidia kukabiliana na uhaba wa madawati katika
shule za umma nchini.
Makabidhiano yalishuhudiwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbas Kandoro
ambaye alisema madawati hayo700 yataboresha mazingira ya kujifunzia kwa
watoto katika wilaya hizo tatu, akitoa wito kwa wadau wengine wenye mapenzi
mema kujitolea na kujiunga kwenye jitihada za kukabiliana na sehemu
iliyobaki ya uhaba wa madawati mkoani humo.
Picha na habari kwa hisani ya
http://bongodailyupdates.blogspot.com/