Kwa waliowahi kupita barabara inayotoka Buguruni kuelekea Tazara jijini Dar es Salaam, bila shaka wameshamuona mkereketwa wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), Shaibu Masaula (46) akiwa ameshikilia bango lenye picha ya mgombea urais wa Chadema Edward Lowassa na mgombea mwenza, Juma Duni Haji huku akirukaruka muda wote.
Hakika ushabiki wa Masaula unawaduwaza watu ambao wamekuwa wakimuona huku wengi wao wakijiuliza maswali mengi pasipo kuwa na jibu, kubwa likiwa nani anayemlipa kwa kazi hiyo?
Masaula anafanya kazi yake hiyo kwa bidii na bila kupumzika wala kuonyesha dalili za kuchoka kwa saa 12.
Iwe jua kali, lipungue au lisiwepo kabisa hababaiki, zaidi huongeza kasi ya kazi yake huku jasho likimtiririka na kulifuta wakati akiendelea kuruka huku akiizungusha picha yake kila pande ili kuwaonyesha wapita njia kwa maana ya kampeni.
Saa 12 kazini
Nilifika eneo hilo saa 11.30 alfajiri, walau nijifunze na kuijua ratiba ya mkereketwa huyu ambaye kila anayemuona kwa mara ya kwanza na hata waliomzoea wamekuwa wakimshangaa.
Saa 11.50, Masaula aliwasili akishuka kwenye daladala inayotokea Mbagala kwenda Ubungo, moja kwa moja alieleka kwenye meza ya kuuzia mitumba iliyo upande wa kushoto mwa barabara, aliinama na kuichukua picha yake kisha kuifuta vumbi.
Ilipotimu saa 12.00 alijongea katikati ya barabara, eneo ambalo magari yanayotoka Buguruni na Tazara yanamuona kisha akaanza kurukaruka akiizungusha picha yake.
Alianza kurukaruka kwa kasi wakati huo alikuwa akiimba kwa sauti bila kutoa maneno, huku akiwa ameinyoosha picha yake juu na alitumia saa mbili kwa hatua hiyo.
Saa 2.00 asubuhi kasi yake ilipungua kidogo na aliiweka mikono yake usawa wa kifua, akaendelea kurukaruka kama anakimbia bila kupumzika wakati huo, nilikuwa nimesimama karibu na eneo lake la kazi nikimuangalia na alijua namshangaa, lakini hakujali chochote.
Saa 2.39 asubuhi aliondoka, akavuka barabara upande wa kulia akaiweka picha yake kwa mama lishe mmoja na kuaga kuwa anaelekea uani ambako hakuchukua hata dakika tano akawa amesharejea.
Bila kuzungumza na mtu, aliichukua picha yake akarejea tena kwenye eneo lake na kazi na kuanza kuruka na aliongeza kasi.
Nilishuhudia wakereketwa wa Ukawa wakimpongeza kwa kazi hiyo na wengine wakimtuza fedha za kununulia maji. Lakini pia walipita wakereketwa wa CCM, hawa walimsihi aachane na kazi hiyo.
Wapo walioonekana kumtolea maneno machafu, kwake hilo halikumtisha, hakujibu lolote na badala yake aliongeza kasi ya kuruka na pale, alipopongezwa,
alitabasamu huku akinyoosha mkono mmoja juu na kuweka alama ya vidole viwili.
Saa 4.00 asubuhi alivuka barabara upande wa kushoto, akaenda kuhifadhi picha yake kwa muuza mitumba mmoja kisha, akajongea mpaka eneo la mama lishe aitwae Mariam Kassim kwa ajili ya kupata kifungua kinywa.
Kifungua kinywa
Masaula aliagiza maandazi saba, kila moja lilikuwa likiuzwa Sh100, maharagwe vipimo viwili kwa bei ya Sh400, maji mawili kwenye kimfuko cha nailoni kila moja Sh100 na kikombe kimoja cha chai kwa Sh200.
Alipoletewa aliinama na kutamka neno Bismillahi, akaanza kula polepole huku akizungumza na wateja wengine.
Nami nilijongea, nikaagiza kikombe cha chai huku nikifuatilia mazungumzo.
Alitumia dakika 10 kupata kifungua kinywa na baada ya kupumzika kama dakika tatu hivi, alikunywa maji na kwenda kunawa mikono yake, kisha moja kwa moja alielekea eneo lake la kazi; kuendelea kuruka ruka akiinadi picha ya Lowassa.
Wakati huo ilishatimu saa 4.20 asubuhi, jua lilikuwa kali lakini kwa Masaula halikuonekana kumzuia kufanya shughuli yake. Aliruka kwa kasi kubwa zaidi ya ile ya asubuhi na wakati huu alianza kutamka neno ‘mabadiliko’ kila anaporuka.
Hakupumzika hadi saa 6.50 ambako alielekea kwa muuza mitumba yuleyule na kumkabidhi picha yake mwenyewe akiaga kwamba anaelekea msikitini kwa ajili ya ibada ya Adhuhuri.
Yeye mbele, mimi nyuma; alipofika msikitini niliketi pembeni nikitazama namna ambavyo anafuata ratiba yake na saa 7.15 mchana, alitoka akanyoosha moja kwa moja hadi kwenye eneo la chakula wakati huu hakuenda eneo lile la chai.
Alikwenda moja kwa moja kwa mama lishe aitwaye Amina Salum ambako aliagiza wali kwa maharagwe uliokuwa ukiuzwa Sh1,500 na maji ya kunywa ya Sh500.
Alitumia nusu saa kupata chakula hicho na kisha alirejea kwenye eneo lake alikokuwa amehifadhi picha yake, akaichukua na kujongea kwenye eneo la kazi na kuanza kurukaruka akiinadi picha yake.
Aliendelea kupata mashabiki ambao walikuwa wakimrushia fedha, aliziokota huku akiendelea kurukaruka. Wapo waliosogea kwa ajili ya kumsemesha, aliwajibu huku akiendelea kurukaruka.
Wakati huo jua lilikuwa kali kiasi cha kuninyong’onyeza lakini kwa Masaula, ni kama halikuwapo, aliendelea na kazi yake ya ajabu.
Saa 10.37 alasiri, alivuka tena barabara hadi upande wa kulia akaiweka picha yake, kwenye eneo la mama lishe, pale alipokuwa ameiweka asubuhi wakati akielekea uani kisha kuaga kuwa angeifuata baada ya muda mfupi.
Kama kawaida hakutumia muda mrefu na akarejea barabarani ambako alianza kuruka ruka wakati huu alikuwa na kasi kubwa zaidi.
Alifanya hivyo hadi saa 1.00 usiku bila kupumzika ambako alitamka neno Bismillahi, kisha akavuka barabara hadi upande ule ambao huhifadhi picha yake kwenye meza za wauza mitumba akaiweka vizuri na kuketi juu ya meza.
Huo ulikuwa wakati muafaka wa kuzungumza na Masaula.
Anajizungumziaje?
“Sijawahi kuwa mwendawazimu kwenye maisha yangu, ninazo akili timamu na ninapanga ratiba yangu kadri Mungu anavyonijalia na ninaimaliza salama,” anasema Masaula.
Mkazi huyo wa Mbagala, Kongowe anasema huwa anaamka saa 10.00 alfajiri kisha anakwenda msikitini na ikishatimu saa 11.20 huanza safari ya kwenda kazini ambako amekuwa akifika kati ya saa 11.40 hadi saa11.50 na kuianza rasmi saa 12.00 asubuhi.
“Nachoka sana na kuna wakati miguu huwa inafukuta kwa maumivu lakini, sitaacha kazi yangu hii ambayo wote walioiga wameshindwa hadi siku ya uchaguzi, sheria itakapozuia kufanya kampeni,” anasema.
Anasema kwa siku amekuwa akikusanya kati ya Sh7,000 hadi 10,000 kulingana na watu watakavyovutiwa na kumtuza fedha ambayo hata hivyo, haitoshi kuendesha maisha yake.
Unaweza kudhani kwamba anapokea mshahara kutokana na kazi hiyo, lakini anasema siyo tu kwamba hakuna chama kinachomlipa kwa kazi hiyo, bali pengine viongozi wa juu hawajui kama kuna mtu anayeshinda juani kufanya kampeni kwa maelfu ya watu wanaotumia barabara ambayo amekuwa akishinda.
“Sijui kama wanajua nipo hapa kwa sababu sijawahi kukutana wala hawajawahi kuja kuniona, hayo yote sijali ninachotaka mimi ni kufikisha ujumbe kwa wananchi tu,” anasema.
Anamshukuru Mungu kwa kumpa nguvu ambazo anasema akianza kurukaruka, huwa hasikii kuchoka na kila dakika zinavyosogea huongeza kasi akitamani jioni isifike kwa sababu usiku hakuna atakayeweza kuiona picha yake.
Katika Ukawa yupo CUF
Masaula ni mwanachama wa Chama cha Wananchi (CUF) na alichojiunga nacho akitokea Chama cha Mapinduzi (CCM).
Anasema amekuwa akifanya kazi hiyo ya kurukaruka na kuonyesha picha ya wagombea wa nafasi ya urais kila mwaka na kwamba mwaka 1995 na 2000 alifanya hivyo kumnadi mgombea urais wa CCM, Benjamin Mkapa.
Mwaka 2002 alihamia CUF na katika kampeni za mwaka 2005 na 2010, alimnadi Profesa Ibrahim Lipumba.
Safari hii, baada ya vyama vinne vya CUF, NLD, NCCR – Mageuzi na Chadema kuungana, Masaula anamnadi Lowassa na alianza kampeni hiyo mara baada ya mgombea huyo kutangazwa.
Ni baba wa familia
Masaula amemuoa Mwanahawa Abdallah na wamejaliwa kupata watoto watatu.
Mtoto wake wa kwanza anasoma darasa la nne katika Shule ya Msingi Mwandege, Mbagala na wengine wawili ni wadogo na hawajaanza shule.
Anasema miongoni mwa vitu vya msingi kwenye maisha yake ni familia ambayo amekuwa akiilea na kuihudumia kupitia kazi yake ya biashara ya mitumba.
“Familia ni ya msingi kwenye maisha yangu, sijawahi kuwaacha wanangu na mama yao wakiwa na njaa. Licha ya kuwa nipo kwenye kazi ya kampeni ila nina kibanda kingine cha mitumba nilichoajiri mfanyakazi, huko ndiko ninakopata fedha za kuendeshea maisha yangu,” anasema.
Kutoka Masasi mpaka Dar
Masaula alifika Dar es Salaam mwaka 1989 akitokea Wilaya ya Masasi, Mtwara akiwa na lengo la kutafuta maisha.
Kwa mara ya kwanza, alipata kazi ya kufanya usafi kwenye kiwanda cha kutengeneza vioo kabla ya kuiacha na kuhamia Kariakoo akiwa mpiga debe wa kuita wateja kwenye duka la nguo.
“Nilikuja Dar es Salaam kutafuta maisha, sijafanikiwa mpaka leo ila sijakata tamaa kwa kuwa bado ninatafuta,” anasema.
Oktoba 24, utakuwa mwisho wake kufanya kampeni kwenye eneo hilo lakini kwa wakati huu ratiba yake itakuwa kama ilivyo.
Baada ya hapo atarejea katika kazi yake ya mitumba akiamini anachokifanya sasa kitakuwa kimemuongezea umaarufu na hivyo kuwa na nafasi ya kupata wateja wengi zaidi.
Wanamsemaje?
Wapo wanaomchukulia kama mtu aliyechanganyikiwa na wengine wanamchukulia kama mkereketwa wa mabadiliko.
“Haiingii akilini mtu kurukaruka huku akiwanadi watu ambao wao wenyewe hawajui kuwa anawanadi,” anasema Mama lishe katika eneo hilo, Emelina Pius.
Baadhi ya wapita njia ambao, wamekuwa wakipita eneo hilo humchukulia kama mtu asiye na kazi ambaye anatumika kunadi sera za chama na wale wanaomchukulia kama mtu anayejituma kwa kazi yake hiyo, wamekuwa wakimchangia.
Lakini nilipopata nafasi ya kuzingumza naye niligundua kuwa ni mtu mwenye akili timamu na asiye na tatizo lolote ukiacha ukereketwa wake wa kiwango cha juu.
Mfanyabiashara maarufu wa eneo hilo, Selemani Said alisema muuza mitumba hiyo ana akili timamu na wakati usio wa kampeni huwa anafanya bishara za mitumba.
“Huyu jamaa ana akili timamu na ni mpole sana ndiyo maana wakereketwa wa vyama vingine wakipita na kumtukana hajawahi kuwajibu lolote isipokuwa wale wanaounga mkono Ukawa, wakimshangilia naye huwa anawajibu huku akiwanyoshea vidole vyake,” anasema.
Masaula anavumilia matusi, kebehi, kejeli, vitisho na wakati mwingine kuzomewa lakini hajawahi kuacha kazi yake ya kurukaruka huku akionyesha picha aliyoibeba mkononi.
chanzo;mwananchi
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia