MGOMBEA urais wa
CHADEMA na UKAWA, Edward Lowassa, jana amefanya mikutano minne ya
kampeni jijini Dar es Salaam na kuvitaja vipaumbele 11 ambavyo
atavitekeleza ndani ya siku 100 baada ya kuchaguliwa.
Amesema asipotimiza vipaumbele hivyo ndani ya siku 100, ruksa wananchi kumuuliza.
Vipaumbele hivyo ni
kuhakikisha Jiji la Dar es Salaam linaondokana na foleni, pili kufuta
michango yote shuleni, tatu elimu bure kuanzia chekechea hadi Chuo
Kikuu, nne kuunda mfumo bora wa kulipa na kukusanya kodi ambao
utaliwezesha Taifa kuongeza mapato yake, tano kukuza michezo na sanaa.
Kipaumbele cha sita ni
kuunda tume ambayo itashughulikia migogoro ya wakulima na wafugaji, saba
kuunda tume ya kushughulikia masilahi ya wafanyakazi, nane kupunguza
kodi katika mishahara ya wafanyakazi, tisa kuboresha masilahi ya
wanajeshi na askari polisi.
Lowassa alisema
kipaumbele cha kumi, atahakikisha anaboresha huduma za afya kwa
akinamama na kuondoa kero wanazopata waendesha bodaboda na mama lishe,
kumi na moja kutengeneza mkakati wa kuondoa tatizo la maji nchini.
"Hivi ndivyo vipaumbele
vyangu, nikiingia Ikulu baada ya siku 100, nitawaeleza Watanzania kama
nimevifanya au la...nimezunguka maeneo mengi na kuona jinsi Watanzania
walivyo na kiu ya mabadiliko; hivyo mwaka huu CCM ni vigumu kurudi
madarakani," alisema.
Frederick Sumaye
Waziri
Mkuu mstaafu aliyehama CCM na kuhamia upinzani, Frederick Sumaye,
alisema Watanzania watajiangamiza wenyewe mwaka huu kama Oktoba 25,
mwaka huu, watairudisha CCM madarakani.
Alisema huu ni mwaka
wao wa kufurahia mfumo wa vyama vingi vya siasa kwa kuiingiza UKAWA
madarakani ili kupata maendeleo na mabadiliko ya kweli.
"CCM wamevunja mikataba
na wananchi ambao wameendelea kuwa na maisha magumu...iliahidi maisha
bora kwa kila Mtanzania, kutoa ajira lakini hadi sasa hawajatekeleza,"
alisema Sumaye.
Alimshangaa Jaji
mstaafu Joseph Warioba aliposema upinzani hawawezi kuweka historia ya
kuiondoa CCM madarakani akimtaka aelewe kuwa, tangu nchi ipate uhuru
wananchi wanaishi kwa shida ambapo hiyo ni historia tosha hivyo lazima
CCM iondoke madarakani.
John Mnyika
Naibu
Katibu Mkuu wa CHADEMA Bara, John Mnyika, alisema wataendelea kuisumbua
Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili iweze kutenda haki katika Uchaguzi
Mkuu ujao.
"Baada ya UKAWA kutoa
taarifa za kinachoendelea ndani ya NEC, Jaji Lubuva anasema tunawabana,
lazima tuendelee kuwabana tukiwatumia wataalamu wetu kwenye mfumo wa
kuhesabia kura na ndani ya sikunne tunataka awe ametupa majibu,"
alisema.
Mama Regina Lowassa
Katika
hatua nyingine, Mama Regina Lowassa, amewataka wanawake nchini
kuyahamasisha makundi mbalimbali ya watu yajitokeze kupigakura ili Taifa
liweze kupata viongozi ambao watajali masilahi ya Watanzania.
Mama Lowassa aliyasema
hayo Dar es Salaam jana kwenye Kongamano la Wanawake wa Wilaya ya
Kinondoni na kuongeza kuwa, kama UKAWA watashinda katika uchaguzi huo,
wataunda Katiba mpya itakayozingatiamaoni ya wananchi, kuondoa sheria
kandamizi kwa wanawake.
Mwakilishi wa Baraza la
Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), Penina Enock, alisema baraza hilo
limefanikiwa kuwaweka wanawake pamoja kutoka vyama vyote vinavyounda
UKAWA.
Freeman Mbowe
Mwenyekiti
wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alisema Oktoba 25, mwaka huu, wanaume wote
walinde kura kwa kukaa mita 100 kutoka kwenye vituo vya kupigia kura na
wanawake warudi nyumbani kuwapikia chakula.
James Mbatia
Naye
Mwenyekiti Mwenza wa UKAWA, James Mbatia, alisema Tanzania bila CCM
inawezekana hivyo kushika dola ni maridhiano na kukitaka Kituo cha
Demokrasia nchini (TCD), kutoa ufafanuzi jinsi watavyokabidhiana
madaraka kama uchaguzi utakuwa huru na haki.
Tundu Lissu
Mwanasheria
wa CHADEMA, Tundu Lissu, alisema UKAWA watashinda kihalali wakitumia
nguvu ya umma, hivyo CCM itoe ratiba ya kukabidhimadaraka.
Mikutano
hiyo minne jana ilifanyika katika Wilaya tatu za jiji ambazo ni Temeke,
Kinondoni na Ilala ambapo kwa Upande wa Temeke, mkutano umefanyika
katika Viwanja vya Mwembe Yanga na Ilala (Uwanja wa Shule ya Msingi
Liwiti-Jimbo la Segerea).
Katika wilaya ya Kinondoni mikutano ilifanyika Tip Top (Sinza) na Tanganyika Packers (Kawe).