Tanzania Kuwa Mwenyeji wa Mkutano wa Kikanda wa Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika 2025

 


Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa,akiongea na waandishi wa habari juu yaMkutano wa Kikanda wa Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika 

Na Woinde Shizza, Arusha


Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa Mkutano wa Kikanda wa Baraza la Viwanja vya Ndege Afrika (Airports Council International – ACI Africa), ambao utafanyika Aprili 2025 jijini Arusha.


Akizungumza na waandishi wa habari leo, Waziri wa Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alisema kuwa tukio hilo litaambatana na Mkutano wa 73 wa Bodi ya ACI Africa pamoja na maonesho ya wadau wa sekta ya anga ,Tukio hili linatarajiwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 300 kutoka nchi 54 barani Afrika.


Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo akiongea na waandishi wa habari 

“Tanzania imepata nafasi hii baada ya kushinda zabuni ya kuwa mwenyeji wa mkutano huu muhimu. Hii ni fursa ya kipekee kwa nchi yetu kuimarisha sekta ya anga, utalii, na uchumi wa taifa kwa ujumla,” alisema Waziri.


Kaulimbiu ya mkutano huo ni “Katika kuelekea Wakati Ujao Bora wa Kijani: Kutumia Usafiri wa Anga Endelevu na Utalii kwa Ustawi wa Kiuchumi”. Waziri Mbarawa aliongeza kuwa mkutano huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa, yakiwemo kuongeza mapato ya fedha za kigeni, ajira kwa wananchi wa Arusha, na kuvutia wawekezaji katika sekta ya anga.



“Pia, mkutano huu utatoa nafasi ya kujadili changamoto za sekta ya anga, kama vile matumizi ya teknolojia ya kijani na njia za kupunguza utoaji wa hewa ya ukaa,” aliongeza Waziri.


Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Abdul Mombokaleo, alisema kuwa mkutano huu ni fursa kubwa kwa nchi kujitangaza na kuvutia wawekezaji. “Watakuja wadau kutoka nchi mbalimbali ambao watasaidia kuunganisha sekta ya anga, kiuchumi na kiutalii, jambo ambalo litaimarisha uchumi wa taifa,” alisema.





Alisem kuwa Kwa ujumla, mkutano huu ni fursa ya kipekee kwa Tanzania kujiongezea nafasi ya ushindani kwenye sekta ya anga barani Afrika huku ikikuza uchumi wa ndani kupitia fursa mbalimbali zinazotokana na tukio hilo kubwa






Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda, alisema kuwa mkutano huu utachochea maendeleo ya uchumi wa mkoa na taifa kwa ujumla ambapo alibainisha kuwa wananchi wa Arusha watanufaika kupitia biashara za mahoteli, usafiri, na huduma nyingine zitakazotolewa wakati wa tukio hilo.


“Ni wazi kuwa kupitia mkutano huu, wananchi wataweza kuona mafanikio yanayotokana na jitihada za serikali yao katika kukuza uchumi na sekta ya anga,” alisema Makonda.





Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post