Baada
ya muda mrefu kupita bila kuwa na tamasha lolote la wanafunzi hasa wa
shule za Sekondari, uongozi wa Mtakuja Secondary School ua Kunduchi kwa
kushirikiana na mtangazaji maarufu Allan Lucky 'Rais wa Wanafunzi' wa
kipindi maarufu cha Skonga ambacho hurushwa kupitia televisheni ya
vijana ya EATV umeandaa tamasha la wanafunzi linalotarajiwa kuhudhuriwa
na wanafunzi zaidi ya 3000 kutoka katika shule zaidi ya 20 za jijini
Dar-es-salaam.
Tamasha
hilo lenye lengo la kuwakutanisha wanafunzi wa shule mbali mbali za
Dar-es-salaam kwa pamoja na kupata changamoto kimawazo na kiburudani,
pia kuwakutanisha wadau mbali mbali wa elimu katika kufanikisha
uboreshwaji wa elimu na kusaidia katika kutekeleza mpango wa 'Matokeo
Makubwa Sasa', linatarajiwa kufanyika Jumamosi ijayo tarehe 14/09/2013
katika viwanja vya shule hiyo.
Miongoni
mwa shule ambazo zitashiriki ni: Mtakuja, Kondo, Jordan, St. Gasper,
Mbezi Beach, Boko, Goba, Twiga, Maendeleo, Mwambao, Kisauke, Kinzudi,
londa, Makongo, Kawe Ukwamani, Tegeta, Mbweni, Teta, Hananasif na
Mtongani, zote ni za sekondari.
Tamasha
hilo linatarajiwa kuhusisha wadau mbali mbali wa elimu watakaokutana
katika kubadilishana mawazo na kupata burudani kwa kushuhudia vipaji
lukuki walivyo navyo wanafunzi kutoka shule mbali mbali.
Miongoni
mwa shughuli zitakazoendeshwa ni pamoja na maswali na majibu, fashion
show, uimbaji, ufokaji, na wanafunzi wenye vipaji mbali mbali maalum
watapewa nafasi.
Msemaji
wa tamasha hilo ambaye pia ni mwalimu wa michezo wa Mtakuja Beach
Sekondari Bw Misonji Charles amewataka wadau mbali mbali wa elimu
kuhudhuria na kushuhudia vipaji vya wanafunzi mbali mbali na pia
amewataka waandishi wa habari kujitokeza kwa wingi katika kuchukua
habari na matukio mbali mbali yatakayojitokeza. Pia amewaomba wadau
mbali mbali wenye uwezo wa kuchangia katika kufanikisha tamasha hili
wajitokeze, kwa kuwa linaandaliwa kwa nguvu za shule na kamati maalum ya
maandalizi pekee.
Kwa maelezo na kama unataka kushiriki, tafadhali wasiliana na Msemaji wa Tamsha Bw Misonji Charles kupitia 0714642442.