Mtoto Mathias Gwaatema Baran (8) mkazi wa Kijiji cha Endamanang, Kata
ya Nar, Wilaya ya Babati Mkoani Manyara, amefariki dunia baada ya kukutwa mwili
wake ukielea kwenye kisima cha maji wakati akichunga mifugo.
Akizungumza na gazeti hili juzi, Ofisa mtenda wa kata ya Nar, Philipo
Mohe alisema mwili wa mtoto huyo Baran ulikutwa ukielea kwenye maji ya
kisima kilichopo katika kijiji hicho.
Mohe alisema awali Baran alitoka asubuhi nyumbani kwao akiwa na
mifugo kwa ajili ya kwenda kuichunga na ilipofika jioni mtoto huyo hakurudi
nyumbani ndipo wazazi wake wakashikwa na hofu.
“Kutokana na hali hiyo wazazi walipiga Ohayoda (yowe) bila mtoto
huyo kuonekana na kesho yake watu waliendelea kumtafuta na kukuta mwili wake
ukielea kwenye maji ya kisima karibu na alipokuwa na mifugo,” alisema Mohe.
Alisema baada ya watu hao kukuta mwili huo kwenye kisima, walitoa
taarifa kwenye ofisi yake na ndipo akawasiliana na polisi waliofika mara moja
kwenye eneo hilo na kuuchukua mwili wake.
Ofisa mtendaji huyo alidai kuwa mwili wa marehemu huyo
umehifadhiwa kwenye hospitali ya mji wa Babati (Mrara) kwa ajili ya uchunguzi
zaidi kuhusiana na tukio hilo.
Hata hivyo, Kaimu Kamanda wa polisi wa mkoa wa Manyara, Mussa
Marambo alidhibitisha kufariki dunia kwa mtoto huyo Baran na kudai kuwa bado
wanaendelea na uchunguzi wa kifo hicho.
“Hadi hivi sasa hakuna mtu anahisiwa kuwa alihusika na kifo hicho,
kwani baada ya kupata taarifa ya kifo hicho tulifika eneo la tukio mara moja na
kuuchukua mwili wa marehemu kwa uchunguzi,” alisema Kamanda Marambo.