DOUBLETREE YAGAWA TAA ZA UMEME JUA ZENYE THAMANI YA TSH 5MILLIONI VISIWANI

Fundo 2
Mkurugenzi wa Mauzo wa Hoteli ya DoubleTree by Hilton Florenso Kirambata akiwaelekeza wanafunzi wa shule ya Msingi Maskul Fundo, Jimbo la Gando kisiwani Pemba jinsi ya kutumia taa za nishati Jua walipotembelea shule hiyo katika moja ya kampeni zake za kugawa taa za nishati mbadala kwa shule za msingi nchini.
Fundo 3
Mkurugenzi wa Kanda wa Hoteli ya DoubleTree by Hilton ya Dar es Salaam Bw. Judd Lehmann akiangalia jinsi mwanafunzi anavyoweza kuwasha taa ya nishati ya Umeme Jua jana visiwani katika jimbo la Gando.
Fundo 1
Wanafunzi wa shule ya Msingi Maskul Fundo, Jimbo la Gando kisiwani Pemba wakiwa wamepozi kwenye picha ya pamoja wakati wa hafla ya kukabidhiwa taa za nishati ya Umeme Jua zilizotolewa na Hoteli ya DoubleTree.
. Ni muendelezo wa kampeni ya nishati ya mbadala
.Lengo ni kusaidia wananchi kuelewa matumizi ya Umeme Jua ambao ni rafiki wa mazingira
.Ni programu ya miaka miwili mashuleni
Hoteli ya Double Tree by Hilton ya jijini Dar es Salaam imeendelea na kampeni zake kabambe ya matumizi ya nishati ya jua kwa kugawa taa 200 kwenye shule ya Msingi Maskul Fundo, Jimbo la Gando kisiwani Pemba, Moblog linaripoti.
Akizungumza kwenye hafla hiyo fupi ya kugawa taa hizo jana, Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo, Ndugu Said Ali Mbarouk ambaye ni Mwakilishi wa Jimbo la Gando, amesema kwamba msaada huo wa Double Tree kwa shule hiyo ni kielelezo tosha kwamba sekta binafsi zina mchango mkubwa katika sekta ya elimu hapa nchini.
“Napenda kuchukua fursa hii adhimu kuwashukuru uongozi na wafanyakazi wote wa Double Tree kwa msaada wao mkubwa kwa shule yetu ya hapa Gando ambapo watoto wetu watasoma katika mazingira rafiki yatayowawezesha kufaulu mitihani yao,’ alisema Mbarouk.
Waziri Mbarouk amesema kwamba kutokana na mabadiliko ya tabia nchi Serikali, wananchi na wadau wote wa maendeleo hawawezi kuendelea kutegemea umeme wa vyanzo vya maji na badala yake umeme wa jua ambao ni nishati mbadala ni ufumbuzi wa tatizo la nishati nchini.
Amesema mchango wa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi hasa kwenye nishati ni muhimu kwa sababu ni nishati ndio injini ya Uchumi wa taifa lolote lile hapa duniani kwa sasa.
‘lakini kampeni hizi zitakuwa msaada mkubwa kwa wanafunzi kutambua na kuelewa nishati mbadala na umuhimu wake katika maisha ya kila siku ikiwemo mazingira,” alisisitiza
Hoteli ya DoubleTree ilizindua rasmi kampeni ya matumizi ya nishati ya jua ambayo itadumu kwa muda wa miaka miwili katika shule za msingi nchi nzima miezi kadhaa iliyopita.
DoubleTree itakuwa ikigawa taa 200 za mezani zenye kutumia nishati ya jua kwa wanafunzi wa darasa la saba kwa shule tofauti kila mwezi, lengo likiwa nikuwafanya wawe na ufahamu zaidi juu ya chanzo kingine cha umeme ambacho ni rafiki wa mazingira kwa kupitia mafunzo katika madarasa yao.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post