WAANDISHI
wa habari sita wamenusurika kufa baada ya gari walilikuwa wakilitumia
kwenye msafara wa wabunge wa Umoja wa Kamati za Mabunge za Hesabu za
Serikali kutoka nchi Wanachama wa SADC (SADCOPAC), kuanguka wakiwa
njiani kuelekea Hifadhi ya Ngorongoro.
Ajali hiyo ilitokea jana
saa 3:30 asubuhi nje kidogo ya mji wa Karatu ambapo waandishi
waliokuwemo na vyombo vyao kwenye mabano ni Veronica Mheta (Habari Leo),
Asraji Mvungi (ITV), Edwin Mjwahuzi (Mwanachi), Peter Nyanje (Citizen),
Deogratius Kasamia (Cluods Tv) na Afisa Habari wa Bunge, Owen
Mwandumbya.
Gari hilo lenye namba za usajili T731 ARL lilikuwa
likiendeshwa na dereva wa kampuni ya uwakala wa utalii Shidolya Tours
& safari aliyejulikana kwa jina moja la Riziki ambaye alipoteza
fahamu.
Kwa mujibu wa waandishi hao, mara baada ya tukio hilo
walipatiwa usafiri wa kuwapeleka mpaka Hospitali ya Wilaya ya Karatu kwa
matibabu ambapo baada ya uchunguzi wengine walionekana wako sawa, hivyo
kuendelea na safari Majeruhi wengine, Kasamia, Oweni, dereva, Riziki na
ofisa usalama ambaye jina lake halikupatikana walipelekwa jijini Arusha
kwa matibabu zaidi baada ya kuonekana wana majeraha.
Kamanda wa
polisi mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas, alisema kuwa alisikia tukio hilo
ingawa bado anasubiri taarifa kamili toka kwa mkuu wa polisi wa wilaya
hiyo ili aweze kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.
Wakielezea
tukio hilo, waandishi hao walisema kuwa gari lao likiwa katika msafara
wa magari zaidi ya 50 yaliyobeba wabunge, askari na wanausalama
lilijaribu kulipita gari lililokuwa mbele ndipo ghafla gari jingine
lililokuwa kwenye msafara nalo lilitoka kwa mwendo kasi likiyapita
magari mengine.
Mheta alisema kuwa hali hiyo ilimfanya dereva wa
gari lao kupoteza muelekeo ambapo alijaribu kuwakwepa waenda kwa miguu
waliokuwa pembeni ya barabara lakini alishindwa kulimudu na hivyo
likapinduka.
Chanzo: Tanzania Daima, Picha zote na Owen David
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia