Mwenyekiti Wa Makampuni ya IPP Reginald Mengi
Na Mwandishi Wetu
MWENYEKITI wa Makampuni ya IPP, Reginald
Mengi amesema Watanzania wengi wanazidi kuwa masikini kwa sababu
hawazitumii fursa za utajiri uliopo nchini, hivyo kutaka vijana kuona
kwa macho fursa hizo ili waweze kujikwamua kutoka kwenye dimbwi hilo la
umasikini.
Akizungumza wakati wa kutoa zawadi kwa
washindi watatu wa shindano la nini kifanyike kuzalisha ajira nyingi
hapa nchini aliloanzisha Mwenyekiti huyo wa IPP, Mengi alisema baada ya
Watanzania kupofushwa kuwa nchi yao ni masikini, wengi walibweteka na
kushindwa kuchangamkia fursa zilizopo hali ambayo imeifikisha nchi hapa
ilipo.
Alisema jambo la msingi kwa vijana wa
Tanzania ni kuibua mawazo ya shughuli gani atafanya badala ya kukimbilia
namna ya kupata mitaji, kwani wengi ambao wamekimbilia kutafuta mitaji
wamejikuta wanaipata mitaji hiyo, lakini wakashindwa namna ya kuitumia.