Malkia
wa Zouk nchini Hafsa Kazinja akiwa na Omari Mkali (kushoto) na Abdul
Salvador baada ya kukamilisha kurekodi wimbo wa 'NIMUOKEOE NANI' katika
Studio za OM Productions jijini Dar es salaam wikiendi hii.
Baada ya ukimya wa muda mrefu, Malkia wa Zouk Tanzania, Hafsa Kazinja, anaibuka upya katika fani akiwa na ingizo lake
la kwanza kati ya kumi aliyoandaa kwa
kuimba wimbo maarufu wa NUTA Jazz Band uitwao “NIMUOKOE NANI” anauouleta hewani katika mahadhi ya Zouk.
Hafsa Kazinja anasema ameamua kurudi
ulingoni kwa kutoa wimbo huo ili kumuenzi Mzee Muhidin Maalim Gurumo ambaye
amestaafu rasmi fani ya muziki baada ya kufanya kazi hiyo akiwa na bendi
mbalimbali tokea mwaka wa 1960.
“Nimeamua kuimba wimbo huu wa “NIMUOKOE
NANI” ili kumuenzi gwiji huyu wa muziki
kwani wakati yeye anastaafu na mimi ndiyo naibuka upya baada ya kukaa kimya kwa
muda”, anasema Hafsa ambaye alitoka kwa wimbo wake wa “PRESHA” aliomshirikisha
Banana Zorro.
Hafsa ameandaa wimbo huo wa “NIMUOKOE NANI”
katika studio za OM Productions ya jijini Dar es salaam chini ya wanamuziki
nguli, Abdul Salvador na Omari Mkali.
“Nafurahi kwamba wimbo wa NIMUOKOE NANI
nimeuimba baada ya kupata Baraka zote toka kwa mtunzi na mwimbaji wake Mzee
Gurumo mwenyewe.
“Haikuwa rahisi kama inavyoweza kudhaniwa
kwani baada ya kwenda kumuona nyumbani kwake alinifanyisha mtihani wa kuuimba
wote kabla ya kuridhika maana alisema asingefurahi kuona wimbo wake unaimbwa
hovyo hovyo na kuharibiwa radha yake”, anasema Hafsa, ambaye hivi sana
anamalizia ngoma zake zingine tisa alizotunga mwenyewe, kabla ya kuvamia anga
kwa mara ingine.
Hafsa anasema katika ukimya wake amekuwa
akifanya utafiti na kujifunza kwa undani zaidi fani ya muziki, akipata mawaidha
maridhawa toka kwa wanamuziki nguli ndani nan je ya nchi wakiwemo Muhidin
Maalim Gurumo, Omar Mkali, Abdul Salvador na Lokassa ya Mbongo wa Congo
aliyekutana na kufanya naye kazi alipokuwa ziarani Marekani hivi karibuni.
Msanii huyu wa kizazi kipya anasema
ataitambulisha rasmi ngoma ya “NIMUOKOE NANI” katika tamasha la kumuenzi Mzee
Gurumo lililopangwa kufanyika OKtoba 1, 2013 katika ukumbi wa Diamond Jubilee
jijini Dar es salaam.
“Natumaini wapenzi wa muziki watafurika kwa
wingi kwenye tamasha hilo name naahidi kuitendea haki ngoma ya “NIMUOKOE NANI”
hivyo wasikose kuja kujionea wenyewe jinsi sie wa kizazi kipya tunavyoweza
kufanya kazi na wakubwa wetu wa kazi, anaongezea Hafsa ambaye pia anaandaa
video yake pamoja na ya ngoma zake zingine mpya.
Mkongwe Abdul Salvador, ambaye alikuwa
mmoja wa waanzilishi wa bendi ya TANCUT
ALMASI YA Iringa iliyotamba na mtindo wake wa “FIMBO LUGODA”, anamtaja Hafsa
kazinja mmoja wa wanamuziki wa kike waliojaaliwa sauti nzuri na kipaji cha hali
ya juu hapa nchini.
“Kwa kuweza kuimba wimbo wa Mzee Gurumo na
kupatia kisawasawa inadhihirisha kwamba Hafsa ni mwanamuziki aliyekomaa maana
si mchezo kuimba nyimbo ya wakongwe kwa ufasaha kama alivyofanya Hafsa.
“Na hii inadhihirisha kwamba uwezekano wa
kizazi kipya na cha zamani kufanya kazi pamoja ni mkubwa sana na sioni kwa nini
isiwe hivyo”, anasema Salvador.
Omari Mkali, aliyetamba na bendi ya CHUCHU
SOUNDS, chini ya marehemu Yusuf Chuchu, naye anamwelezea Hafsa Kazinja kama
moja ya majembe ya muziki hapa nchini kwa upande wa kinamama, na kwamba anaweza
kufika mbali endapo kama moto aliokuja nao upya atauendeleza.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia