Ticker

6/recent/ticker-posts

TANNESCO KIAMA MABADILIKO MAKUBWA KUFANYIKA ASEMA KIKWETE

 

Rais Jakaya Kikwete, amesema serikali yake inalifanyia mageuzi muhimu na marekebisho makubwa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kwa nia ya kuharakisha jitihada za serikali kusambaza umeme kwa wananchi wengi zaidi.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana alipokutana na kuzungumza na ujumbe wa Shirika la Misaada ya Maendeleo la Marekani la Millennium Challenge Corporation (MCC) ukiongozwa na Mtendaji Mkuu wake, Daniel Yohannes.

Yohannes alimwelezea Rais Kikwete kuhusu maendeleo ya ombi la Tanzania kuingizwa katika awamu ya pili ya misaada ya Serikali ya Marekani kupitia MCC chini ya Akaunti ya Milenia Tanzania (MCA(T)).

Nchi nyingine za Afrika ambazo maombi yao yanafikiriwa katika awamu hiyo ya pili ni Morocco, Msumbiji na Lesotho.
   
Tanzania ndiyo nchi iliyopokea sehemu kubwa zaidi ya msaada wa MCC duniani katika awamu ya kwanza ambapo ilipewa dola milioni 698 za Marekani.

Fedha hizo zimeingizwa katika miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara, usambazaji wa umeme vijijini, miradi ya maji na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Mafia.

Serikali ya Tanzania imeamua kuwa fedha za awamu ya pili ya MCC, zitaingizwa kupanua zaidi huduma za umeme na ujenzi wa barabara za vijijini kwa nia ya kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata huduma za umeme na kwa nia ya kuboresha barabara za vijijini katika maeneo yanayozalisha mazao kwa wingi zaidi.

Serikali imeliweka suala la usambazaji umeme kwa Watanzania mijini na vijijini miongoni mwa maeneo yake ya kipaumbele.

Wakati anaingia madarakani mwaka 2005, ni asilimia 10 tu ya Watanzania waliokuwa wanapata umeme.

Yohannes alitaka kujua ni hatua zipi serikali inazichukua kurekebisha changamoto zinazoikabili Tanesco na hatua zinazochukuliwa kuzidi kukabiliana na matatizo ya rushwa.

Rais Kikwete alimweleza Yohannes: “Kama unavyojua, Tanesco imepitia safari ngumu na kukabiliwa na changamoto nyingi, lakini sasa tumeamua katika serikali kulifanyia mageuzi muhimu na marekebisho makubwa kwa maana ya muundo wake na pia kuangalia viwango vya malipo ambayo shirika hilo linawatoza wateja wake. Mageuzi haya katika Tanesco ni muhimu sana na yameanza kufanyika na kwa hakika serikali imedhamiria kukayamilisha mageuzi hayo katika muda mfupi iwezekanavyo.”
 

Post a Comment

0 Comments