Maafisa wa usalama wakizingira jengo la Westgate jijini Nairobi
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Kenya Joseph Ole Lenku
amesema idadi rasmi ya watu waliopoteza maisha imefikia 59 wakati
majeruhi 175 wakitawanywa katika hospitali mbalimbali jijini Nairobi
kupatiwa msaada wa kiafya.Aidha Ole Lenku ameeleza kuwa wanausalama bado
wanazingira jengo la Westgate kuhakikisha watu waliotekwa na wapiganaji
wa Alshabab wanaokolewa salama na watuhumiwa hao wanatiwa nguvuni.
Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta ametoa pole kwa jamaa waliopoteza
ngudu zao katika tukio hilo na kuwataka raia wa Kenya kushikamana na
kutoa ushirikiano wa hali na mali kwa wanausalama kukabiliana na tatizo
hilo.
Wanamgambo hao wa kundi la kigaidi la Al Shabab wamesema walitekeleza
shambulizi hilo kwa sababu serikali ya Kenya imekataa kuyaondoa majeshi
yake nchini Somalia.
Tayari watu wengine wanne wametajwa na vyombo vya habari nchini humo
kuokolewa kutoka ndani ya jengo hilo la biashara ambapo walishuhudia
kuwa waliwaona watu waliokuwa wamejifunika nyuso zao wakianza
kumshambulia mtu yeyote waliyekutana naye ndani ya jengo hilo jumamosi
mchana.
Inadaiwa kuwa washambulizi hao walikuwa wanamuuliza waliyekutana naye
maswali ya Kislamu na yeyote aliyeshindwa kutoa jibu au kuthibitisha
kuwa ni Mwislamu alipigwa risasi.
Rais Kenyatta ametaja shambulizi hilo la kigaidi kuwa ni kitendo
ambacho hakikubaliki kamwe na waliohusika watakumbana na mkono wa
sheria.
Aidha, Kenyatta amesisitiza kuwa wakenya hawatagawanyika kutokana na
shambulizi hilo na jeshi lake litaendelea kukabiliana na magaidi nje na
ndani ya taifa hilo.
Makundi mbalimbali nchini humo yamejitokeza kulaani shambulio hilo na
kutoa pole kwa wahanga,akiwemo waziri mkuu wa zamani Raila Odinga
ambaye ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuingilia kati mapambano
hayo yanayoendelea nchini humo.
Waziri wa Mambo ya nje wa Ungereza William Hague amesema kuwa
serikali yake inashirikiana na Kenya kuhakikisha kuwa inakabiliana na
suala la ugaidi na wanamgambo hao wanapatikana.
Miongoni mwa raia wa kigeni waliopoteza maisha yao katika shambulizi hilo ni pamoja na raia wawili wa Ufaransa na Canada.
Hili ndilo shambulizi baya zaidi kuwahi kuikumba Kenya tangu
shambulizi la bomu lililotokea mwaka 1998 lilotekelezwa na Al-Qeada.