Mkazi wa Kitongoji cha Kilimahewa,
Kata ya Endiamtu, Mji mdogo wa Mirerani Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara,
amenusurika kufariki dunia baada ya kuungua moto akiwa ndani ya nyumba yake.
Kaimu Kamanda wa polisi wa
mkoa wa Manyara, Kamishna Msaidizi Mussa Marambo alimtaja mtu huyo
aliyejeruhiwa na moto kuwa ni Ester Kiwelu (36) mkazi wa Endiamtu wilayani
Simanjiro.
Kaimu Kamanda Marambo
alisema tukio hilo lilitokea saa 7 mchana, kwenye
kitongoji cha Kilimahewa ambapo Kiwelu alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili
wake kutokana na kuunguzwa na moto huo.
Alisema kuwa siku ya tukio
hilo, walipata taarifa kutoka kwa raia kuwa kuna nyumba inaungua na ndani kuna
mtu huku mlango ukiwa umefungwa, ndipo wakafika eneo hilo na kukuta watu
wamevunja mlango na kumtoa Kiwelu.
“Hadi hivi sasa Kiwelu
amelazwa Tengeru, kwenye hospitali ya halmashauri ya wilaya ya Meru na polisi
bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo kwani chanzo cha moto huo bado
hakijajulikana,” alisema Kamanda Marambo.
Hata hivyo, baadhi ya
wakazi wa eneo hilo walidai kuwa mkazi huyo ambaye inasemekana mara kwa mara
anakuwa na ugonjwa wa akili, inadaiwa kuwa alijifungia ndani na kuwasha moto
huo wa lengo la kujiunguza na moto.
“Huyu mwanamke huwa ana
matatizo ya akili, kwani mwezi ukiwa mchanga anaharibikiwa na kichwa hivyo siku
hiyo aliwasha moto kwa ajili ya kujimaliza na moto huo,” alisema mkazi mmoja wa
eneo hilo.