MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, amewataka
Watanzania kujenga utamaduni wa kutumia nishati mbadala kwa uzalishaji badala
ya kutegemea serikali kusambaza umeme kutoka katika gridi ya taifa.
Mulongo alitoa kauli hiyo jana kwenye hafla ya
kumkaribisha mteja wa 1,000, aliyefungiwa mtambo wa nyumbani wa umeme wa jua wa
Kampuni ya Mobisol kutoka Ujerumani iliyofanyika mkoani hapa.
Alisema serikali kwa kushirikiana na wadau
mbalimbali kupitia Wakala wa Umeme Vijijini (REA) wameweka malengo kuhakikisha
sehemu zote zilizo nje ya gridi ya taifa zinapata nishati ya umeme.
“Ninawapongeza Mobisol kwa kushirikiana na Vodacom
kwa kuwawezesha Watanzania hasa wa maeneo ya vijijini kupata nishati ya umeme.
Ninatoa wito kwa Watanzania kutumia fursa hii kupata nishati kuliko kutegemea
serikali ifikishe umeme katika maeneo yao kutoka katika gridi ya taifa,”
alisema.
Ofisa Mahusiano wa REA, Jaina Msuya, alisema wakala
huyo amefurahia ushirikiano huo ambao umewezesha Watanzania zaidi kupata
nishati ya umeme, hivyo wao kama wakala wako tayari kushirikiana na wadau
mbalimbali kwa kutoa ruzuku ambazo zitawawezesha kufikisha umeme vijijini.
“REA ni moja ya taasisi za serikali zinazotekeleza
mpango wa serikali wa matokeo makubwa, hivyo mafanikio haya ni moja ya
mafanikio ya utekelezaji wa mpango huo,” alisema Jaina.
Mteja wa 1,000 wa Mobisol, Catherine Peter,
alieleza kufurahi kumiliki mtambo wake unaotumia nishati ya umeme wa jua.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia