Wajumbe wa Mkutano
Mkuu wa Dayosisi ya Mbulu, Sinodi ya 41 ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), umemchagua Mchungaji Nicolaus Nsanganzelu (58) kuwa Askofu
mteule wa Dayosisi hiyo.
Mchungaji
Nsanganzelu aliyechaguliwa juzi mji mdogo wa Haydom wilaya Mbulu, anashikilia
nafasi hiyo baada ya aliyekuwa askofu wa Dayosisi hiyo, Zebedayo Daudi (60)
kustaafu uongozi wake.
Akitangaza
matokeo ya uchaguzi huo uliowashirikisha wajumbe 141 Askofu wa dayosisi ya Pare, Charles Mjema alisema
Mchungaji Nsanganzelu amefanikiwa kuwa Askofu baada ya kupata asilimia
97.9 ya kura zote.
Akizungumza baada
ya kutangazwa matokeo hayo Askofu mteule huyo alisema anamshukuru Mungu kwa
kumpa nguvu ya kukubali nafasi hiyo kwani awali aliona amepewa jukumu kubwa
lililo juu ya uwezo wake.
“Hata kwenye
upigaji kura nilijipigia kura ya hapana na nawashukuru wenzangu wengine wawili
walioniunga mkono kwa kupiga kura ya hapana japokuwa Mungu amependa nishikilie
nafasi hii,” alisema Askofu Nsanganzelu.
Naye, Mkuu wa
Jimbo la Haydom na Mchungaji kiongozi wa Kanisa la Haydom, John Nade
alichaguliwa kuwa Askofu msaidizi wa Dayosisi ya Mbulu Sinodi ya 41 kwa kupata
kura zote 141 za wajumbe wa mkutano huo.
Mchungaji Nade
alisema aliombwa agombee nafasi hiyo ila yeye binafsi hakupenda, siyo kwa maringo
au ujivuni wa kibinadamu ila aliona ni majukumu makubwa ambayo asingestahimili
kuyatekeleza.
“Hata hivyo
niliona nakuwa sawa na Yona ambaye aliikimbia kazi ya Mungu na kumezwa na
samaki na mimi kwa moyo mkunjufu kabisa tushirikiane wote tukimtanguliza Mungu
tutaweza kumtumika,” alisema Mchungaji Nade.