Hata hivyo, taarifa ya Interpol ilisema kuwa
alikuwa anatakiwa kujibu mashtaka ya kumiliki mabomu na kupanga njama za
ugaidi Desemba 2011.
Interpol haikuhusisha maombi hayo ya Serikali ya Kenya na mashambulizi ya Nairobi.
Pia Lewthwaite inasemekana aliingia nchini humo kwa kutumia mpaka wa Tanzania.
Baadhi ya vyombo vya habari vya Afrika ya Kusini,
vinasema mwanamke huyo alitumia pasi ya kusafiri ya nchi hiyo kuingia
Kenya kwa kutumia mpaka wa Namanga uliopo mkoani Arusha.
Taarifa hizo zinasema mwanamke huyo alitumia mpaka
wa Lunga Lunga na Namanga kati ya Februari na Agosti mwaka 2011
akitumia jina la Webb.
Habari hizo zinaeleza kuwa, awali mwanamke huyo
alikuwa anaishi Afrika Kusini ambako aliweza kukopeshwa fedha benki na
kuweza kupanga sehemu ya kuishi.
Wakati huohuo, watu wanaodhaniwa kuwa magaidi
wamefanya shambulio kwenye Kituo cha Polisi mjini Mandera na kuua askari
wawili, kujeruhi watatu kisha kuchoma zaidi ya magari 11 jana asubuhi.
Shambulio hilo ni la pili kufanyika kwenye maeneo
mawili tofauti ndani ya saa 24, baada ya lingine lililofanyika kwenye
Mji wa Wajir, muda mfupi baada ya taarifa za kudhibitiwa kwa watu
wanaodhaniwa kuwa magaidi walioshambulia jengo la kibiashara la Westgate
mjini Nairobi.
Shambulio hilo limefanyika wakati kikosi maalumu
cha wataalamu wa mabaki ya mabomu wa Kenya na wale wa kimataifa kikianza
kufanya upekuzi wa jengo hilo, ili kubaini wahusika halisi wa shambulio
hilo na aina ya silaha zilizotumiwa.