BREAKING NEWS

Tuesday, November 10, 2015

HEKTA 400,000 HUPOTEA KILA MWAKA KUTOKANA NA UKATAJI MITI NA KILIMO CHA KUHAMA HAMA

MRATIBU wa programu ya misitu kutoka shirika la hifadhi ya maliasili
na mazingira duniani  (WWF) ofisi ya Tanzania ,Isaac Malugu amesema
kuwa, hekta  400,000 za misitu zinapotea kila mwaka kutokana na
ukataji miti na kilimo cha kuhamahama na hivyo kusababisha uharibifu
mkubwa wa mazingira.

Alisema kuwa, hali hiyo imechangiwa pia na shughuli za kibinadamu
zinazofanywa kila siku ambapo asilimia kubwa ya nishati inayotumika
hapa nchini inatokana na misitu , hivyo elimu zaidi inahitajika kwa
jamii ili kuokoa upotevu huo.

Malugu alisema kuwa,karibu mikoa yote Tanzania imeathirika na upotevu
huo hali inayochangia kuendelea kuwepo  kwa hali ya  ukame katika
maeneo mengi ,ambapo kwa mikoa ya kusini bado ina rasilimali ya
misitu.

Malugu aliongeza kuwa, shirika hilo limeanzisha utafiti wa kuangalia
dhamani halisi ya misitu katika kuhakikisha kuwa inaboreshwa ambapo
utafiti huo utaanza rasmi mwezi huu.

Alifafanua kuwa, katika kuhakikisha wananchi wanatambua umuhimu wa
kuilinda misitu na kuitunza wamewezesha jamii kutambua umuhimu wa
kutunza misitu kwa kutumia nishati nyingine mbadala badala ya ukataji
miti huku wakielimishwa umuhimu wa  upandaji miti kwa manufaa yao.

‘pia tumeweza kuwashirikisha wananchi katika miradi mbalimbali ya
utunzaji wa misitu huku tukiwawezesha kuwekeza katika misitu hiyo ili
wao wenyewe waweze kuwa walinzi wa rasilimali zao na hivyo kuweza
kuokoa upotevu wa misitu unaofanyika kila wakati.’alisema Malugu.

Naye Dokta Sware Semesi kutoka shirika hilo kwa Tanzania,alisema kuwa
,uwekezaji katika misitu bado ni mdogo sana ambapo elimu zaidi
inaendelea kutolewa kuhakikisha wananchi wanatambua umuhimu wa misitu.

Alisema kuwa, elimu zaidi imekuwa ikitolewa  kwa wananchi katika
usimamizi shirikishi wa misitu ili kwa pamoja waweze kushiriki katika
miradi mbalimbali ya misitu na hatimaye kuweza kufaidi matunda
yatokanayo na misitu kupitia mpango shirikishi wa misitu .

Mkurugenzi wa shirika la hifadhi la wanyamapori Afrika(AWF) ,John
Salehe alisema kuwa, wadau mbalimbali kwa ujumla wanahitaji
kuunganisha nguvu kwa pamoja kuhakikisha kuwa wanafanya kazi kwa bidii
na kwa umoja ili utunzaji wa misitu uweze kuwa endelevu.

Salehe alisema kuwa, changamoto kubwa iliyopo katika sekta ya
maliasili ni pamoja na Wizara hiyo kupewa fedha kidogo sana na
serikali ambazo hazitoshelezi  kuendeleza miradi ya utunzaji wa misitu
, hivyo aliitaka serikali kutoa fedha za kutosha kwa wizara hiyo ili
kuendeleza na kuboresha miradi zaidi.
Habari na Woinde shizza,Arusha

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates