BREAKING NEWS

Thursday, August 11, 2022

VIKUNDI 110 VYANUFAIKA NA MIKOPO YA 10% MAPATO YA NDANI ARUSHA DC 2021/2022.

 Na Elinipa Lupembe


Jumla ya vikundi 110 vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, halmashauri ya Arusha, wamenufaika na mikopo siyokuwa na riba inayotokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa mwaka wa fedha uliomalizika 2021/2022.


Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, Mkuu wa Idara ya Maendeleo ya Jamii, Angela Mvaa, amefafanua kuwa, kwa mwaka wa fedha uliopita 2021/2022, halmashauri imeweza kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 781.6 na kuvifikia jumla ya vikundi 522 sawa na 87.5%, kutoka kwenye makisio ya shilingi milioni 209.1 zilizopangwa kukopeshwa kwa mwaka wa fedha 2021/2022 ikiwa ni ongezeko la asilimia 49. kulinganisha na shilingi milioni 384 zilizokopeshwa kwa mwaka wa fedha 2020/2021.


"Kumekuwa na ongezeko la vikundi kuomba mikopo inayotolewa na serikali kupitia halmashauri, hii ni kutokana na ushirikishwaji baina ya wananchi, viongozi, wadau pamoja na kazi kubwa inayofanywa na Maafisa Maendeleo ya Jamii kuanzia ngazi ya kata, jitihada ambazo zimewawezesha wananchi wengi kuwa na uelewa mpana unaowawezesha kutumia fursa hii adhimu ya kupata mikopo hiyo, hata hivyo jumla ya vikundi 522 vilifikiwa na kupatiwa mafunzo ya mikopo na ujasiriamali" Ameweka wazi Mvaa


Mvaa ametoa mchanganuo wa fedha hizo zilizotolewa kwa mwaka huo wa fedha kiasi cha shilingi milioni 781.6, kuwa  jumla ya shilingi milioni 601 zimetolewa kwa vikundi 84 vya wanawake, milioni 170 kwa vikundi 20 vya vijana, na milioni 10.6 watu 6 wenye Ulemavu kwa kata zote 27 za halmashauri ya Arusha.


Nao vijana wa kikundi cha Harmony Youth Group, kata ya Moivo, wanaojishughulisha na ushonaji wa nguo za shule 'school uniform' wamekiri kunufaika na mikopo hiyo isiyokuwa na riba inayotolewa na serikali kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri, mikopo ambayo hapo awali hawakuwa na ufahamu mzuri juu ya mikopo hiyo.


Mwenyekiti wa Kikundi cha Harmony Youth Group, Janeth Mollel amesema kwa kikundi chao kimenufaika na mikopo hiyo kwa kukopeshwa kiasi shilimgi milioni 10, fedha ambazo zimewawezesha kupanua mradi wao wa ushonaji kwa kununua mashine za kisasa na kuipandisha hadhi kazi yao na kuwa na hadhi ya kiwanda kidogo.


"Tulikuwa na mradi wa kushona, tuliouanzisha kwa kuchangishana pesa, na tulikuwa tunashona kwa mashine za kawaida, baada ya kupata mkopo tumenunua mashine za kisasa, na sasa tunajipambanua kuwa na kiwanda kidogo, ambacho kimetuwezesha kupata kazi nyingi za ushonaji wa uniform tofauti na hapo awali". Amefafanua Mwenyekiti Janeth.



Serikali imeendelea kutekeleza mpango wa kuwawezesha wanachi kiuchumi kwa kutoa mikopo isiyokuwa na riba, kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmasahuri zake, mikopo ambayo imeleta matokeo chanya katika kuwawezesha wananchi kujiongezea kipato kwa maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla.

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates