BREAKING NEWS

Thursday, August 4, 2022

UMITASHUMTA WAENDA SAMBAMBA NA SENSABIKA



Na Shamimu Nyaki - WUSM

 Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abbasi amesema wizara hiyo imebuni Kampeni maarufu kwa sasa nchini ya SensaBika ambayo lengo lake ni kuhamasisha wananchi kushiriki Sensa ya Watu na Makazi mwaka huu 2022. Dkt. Abbasi ameeleza hayo Agosti 04, 2022

 Tabora katika Ufunguzi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA ambapo amesema kuwa, wizara hiyo ndio nguvu shawishi ya Taifa pamoja na kutoa furaha kwa watanzania, imeanzisha Kampeni hiyo kutokana na wadau wake wengi kuwa na ushawishi katika jamii ambao wataweza kuhamasisha watanzania kushiriki zoezi la Sensa. 

"Sisi ni wizara ya kutoa furaha na kupitia sekta zetu tuna wadau wengi ambao wakitumia Kampeni hii kupitia umaarufu na ushawishi walionao kwenye jamii itarahisisha kufikisha ujumbe kwa haraka zaidi kwa jamii kushiriki Sensa", amesema Dkt. Abbasi. 


Dkt. Abbasi ametumia nafasi hiyo kumuongoza Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe.Kassim Majaliwa pamoja na Viongozi, Wanamichezo na Wananchi waliohudhuria ufunguzi huo kucheza kibwagizo maarufu sana nchini cha SensaBika.

Wakati huo huo Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe amesema mashindano ya michezo kwa shule za Msingi (UMITASHUMTA) mwaka 2022 yameshirikisha Wanafunzi zaidi ya 3000 kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara na miwili kutoka Zanzibar. 

Ameyazungumza hayo leo Agosti 4, 2022 mkoani Tabora katika hafla ya Uzinduzi wa mashindano hayo yaliyofanywa na Mhe. Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu wa Tanzania. Prof. Shemdoe ameeleza kuwa wanafunzi wanaoshiriki mashindano hayo Wana vigezo na wameandaliwa vizuri kuanzia ngazi ya shule. 

"Mashindano haya yalianza mwaka 2000 ambapo lengo lake ni kukuza vipaji vya Wanafunzi na kuimarisha upendo, ushirikiano na kuboresha afya kwa Wanafunzi", amesema Prof. Shemdoe.

 Ametumia nafasi hiyo kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuendesha shughuli za michezo nchini.

 Mashindano ya UMITASHUMTA yatahitimishwa Agosti 08 mwaka huu na Agosti 9,2022 yataanza mashindano ya UMISSETA. 



Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates