BREAKING NEWS

Wednesday, August 10, 2022

AUWSA YAFIKIA ASILIMIA 68 UTOAJI HUDUMA YA MAJI ARUSHA

 


Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Arusha (AUWSA), Mhandisi Justine Rujomba  akizungumza katika mkutano na vyombo vya habari katika Idara ya Habari- Maelezo jijini Dodoma Agosti 10, ambapo pamoja na mambo mengine amesema kuwa  katika utoaji huduma ya maji Arusha hadi sasa wamefikia  asilimia 68. 

Amesema kuwa mahitaji halisi ya maji kwa sasa ni lita 124,789,000 kwa siku kwa mchanganuo ufuatao; Jiji la Arusha lita 109,689,250, na lita 15,099,750 katika miji midogo. Maji yanayozalishwa kwasasa ni lita 84,500,000 kwa siku kutoka kwenye vyanzo vya visima virefu, chemchem na mito sawa na asilimia 68% ya mahitaji. Matarajio ni kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini kulingana na lengo lililowekwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kabla ya kufika mwaka 2025.


Kwa maelezo zaidi soma taarifa kamili hapo chini...


Afisa Habari Mwandamizi wa Idara ya Habari -Maelezo, Jonas Kamaleki akimkribisha Mkurugenzi wa AUWSA, kuzungumza na vyombo vya habari.
 

Wanahabari wakiwa makini kusikiliza wakati wa mkutano huo.

PICHA ZOTE NA RICHARD MWAIKENDA


TAARIFA YA UTEKELEZAJI WA SHUGHULI ZA MAMLAKA NA MWELEKEO WA UTEKELEZAJI KWA MWAKA 2022/2023.


Utangulizi

Ndugu wanahabari,

Mamlaka ya majisafi na usafi wa mazingira jiji la Arusha (AUWSA) ni Taasisi ya Serikali inayofanya kazi zake chini ya Wizara ya Maji. Mamlaka hii ilianza kufanya kazi Julai 1, 1998 baada ya kuanzishwa na sheria ya maji ya mwaka 1997 iliyobadilishwa na Sheria ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Na. 5 ya Mwaka 2019 ikiwa na majukumu ya kuhakikisha inatoa huduma bora za majisafi na uondoaji wa majitaka kwa ufanisi na kwa uhakika kwa kutumia rasilimali na teknolojia iliyopo kwa maendeleo endelevu ya Jiji la Arusha na Tanzania kwa ujumla. Mamlaka imeendelea kupanua huduma baada ya kuongezewa maeneo ya kutoa huduma ikiwamo kata saba za Wilaya ya Arumeru, pamoja na miji midogo ya Longido, Monduli, Ngaramtoni na Usa River.

Mahitaji halisi ya maji kwa sasa ni lita 124,789,000 kwa siku kwa mchanganuo ufuatao; Jiji la Arusha lita 109,689,250, na lita 15,099,750 katika miji midogo. Maji yanayozalishwa kwasasa ni lita 84,500,000 kwa siku kutoka kwenye vyanzo vya visima virefu, chemchem na mito sawa na asilimia 68% ya mahitaji. Matarajio ni kufikia asilimia 95 ya upatikanaji wa maji mijini kulingana na lengo lililowekwa katika Ilani ya Chama Cha Mapinduzi kabla ya kufika mwaka 2025.

Hali ya Huduma ya Majisafi na uondoaji majitaka pamoja na miundombinu yake.

Ndugu wanahabari,

Kabla ya uwekezaji wa Serikali kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa, uzalishaji wa maji ulikua ni wastani wa lita 40,000,000 kwa siku na huduma ya uondoaji wa majitaka ilikua ni wastani wa asilimia 7.6 ya wakazi wa Jiji la Arusha.

Serikali kupitia fedha za mkopo wa riba nafuu kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imewekeza katika kuboresha hali ya upatikanaji wa huduma ya majisafi na uondoaji wa majitaka katika jiji la arusha. Hadi Julai 2022 utekelezaji wa mradi mkubwa umefikia asilimia 90. Kupitia utekelezaji wa mradi huu, wananchi wa Arusha wameanza kunufaika na vipengele vya mradi vilivyokamilika kama ifuatavyo;

Kiwango cha uzalishaji maji kimeongezeka kwa lita 26,000,000 kwa siku. Ongezeko hilo limewezesha kuboresha upatikanaji wa maji kwenye maeneo yaliyokuwa na uhaba wa maji hasa katika maeneo ya Moshono, Kiserian, Murrieti, Olasiti, Sombetini, Kwa Moromboo, Olmoti, Sokoni 1, na baadhi ya maeneo ya Terati. Ongezeko hili limechangia kuongeza saa za huduma kutoka masaa 15 hadi 19;

Mamlaka kupitia utekelezaji wa mradi wa upanuzi wa mtandao wa majitaka na ukarabati wa mtandao wa zamani imefanikiwa kufanya maunganisho mapya 4,790 ya wateja wa majitaka;

Mamlaka kupitia utekelezaji wa Mamlaka kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa imefanikiwa kufanya ukarabati na upanuzi wa mtandao wa majisafi kwa kilomita 600.


⦁ Majitaka yanatibiwa kwa asilimia 100% kuendana na viwango vya TBS baada ya ujenzi wa mabwawa 18 ya kutibu majitaka kukamilika eneo la Terati; 


⦁ Kupitia utekelezaji wa mradi mkubwa, Mamlaka imefanikiwa kufunga Mtambo wa kupima utendaji kazi wa Dira ‘Water Meter Testing Bench’. Mtambo huu unatumika kupima na kurekebisha dira za wateja zenye changamoto mbalimbali ili kuondoa malalamiko ya wateja kuhusu ufanisi na utendaji kazi wa dira;


⦁ Mamlaka imeweza kuongeza vitendea kazi kama magari, pikipiki pamoja na mitambo mbalimbali na kuongeza ufanisi wa utendaji. 


⦁ Mradi umesaidia upatikanaji wa ajira kwa watu takribani 2,000 kati yao watu 200 ni kutoka nje ya nchi na watu 1,800. kutoka ndani ya nchi. 


⦁ Hadi kufikia mwezi Juni, 2022 wakandarasi wanaotekeleza Mradi mkubwa wameweza kununua vifaa kwenye viwanda vyetu vya ndani na maduka yetu ya jumla vyenye thamani ya Shilingi za Kitanzania Bilioni 140;


⦁ AUWSA imeajiri watumishi 45 wa kada mbalimbali; na


⦁ Hadi mwezi Juni 2022, mradi umewanufaisha wananchi 1,064 kwa kuwalipa fidia kiasi cha Shilingi 5,790,793,407 kwa kutwaa maeneo yao kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya mradi mkubwa. Ulipaji wa fidia kwa maeneo mengine ya mradi unaendelea.


Ndugu wanahabari,


Kwa ujumla, kutokana na juhudi mbalimbali zinazoendelea kufanyika kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika jiji la Arusha na Miji midogo ya Longido, Usa River, Monduli na Ngaramtoni, AUWSA imefanikiwa kufanya yafuatayo;


⦁ Kuongeza kiwango cha upatikanaji wa huduma ya majisafi: Mamlaka imeweza kuongeza upatikanaji wa huduma za majisafi kutoka asilimia 66.8 ya wakazi wa Jiji la Arusha mwaka 2020/21 hadi asilimia 75 mwaka 2021/22. Aidha wateja waliounganishiwa huduma ya maji wameongezeka kutoka wateja 71,183 Juni 2021 hadi wateja 95,748 Juni 2022. Mamlaka inaendelea kuongeza mtandao katika maeneo mbalimbali ya utoaji huduma ili kuweza kufika malengo ya Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kufikia asilimia 95 mijini ifikapo mwaka 2025;


⦁ AUWSA imefanikiwa kutumia mfumo wa GIS kutunza kumbukumbu ya mtandao wote wa maji pamoja na maunganisho ya wateja ili kurahisisha utambuzi wa mtandao.


⦁ AUWSA inaendelea kupambana na upotevu wa maji kwa kutoa elimu juu ya utunzaji wa miundombinu ya majisafi na kuepukana na wizi wa maji kwa kutoa taarifa ya wizi pamoja na uharibifu wa miundombinu ya majisafi kupia kituo cha huduma kwa wateja.


⦁ AUWSA imendelea kupokea na kufanyia kazi changamoto zote zinazowasilishwa kwa simu na wateja kupitia namba ya bure 0800 110 069 ya kituo chake cha huduma kwa mteja (AUWSA Call centre) inayofanya kazi saa 24, kwa siku zote.


⦁ AUWSA imefanikiwa kuongeza mtandao majitaka (sewerage coverage) katika jiji la Arusha kutoka asilimia 8.03 mwaka 2020/21 hadi asilimia 24 mwaka 2021/22. Vilevile, ili kuwafikia wananchi ambao bado hawajajiunga kwenye mtandao wa majitaka AUWSA kwa sasa inatoa huduma ya uondoaji majitaka kwa kutumia gari za majitaka “Sewer Bowsers” Mamlaka inajumla ya gari tano (5) za majitaka, (Gari mbili za ujazo wa Lita 5,000 na gari tatu za ujazo wa lita 10,000). Aidha, AUWSA imejenga vyoo 39 kwenye maeneo yenye mikusanyiko ya watu (masoko, shule na stendi za mabasi). Mamlaka kwa kushirikiana na Shirika la SNV la Uholanzi imekamilisha ujenzi wa mtambo wa kutibu tope kinyesi katika eneo la Murieti, Mtambo huu utasaidia kupokea na kuchakata majitaka yanayobebwa na magari ya majitaka kutoka sehemu mbalimbali za Jiji la Arusha;


⦁ Kwa kupitia fedha za ndani TZS milioni 651 AUWSA imefanikiwa kutekeleza mradi wa upanuzi wa mtandao eneo la Usa River, Kujenga chanzo cha Kibola kinachosambaza maji Momela, Arudeko na Bondeni pamoja na kuboresha tanki la DikDik, Magadirisho na Kilimani ambapo zaidi ya wateja 4,800 wanaunganishiwa huduma ya maji; 


⦁ AUWSA imefanikiwa kukamilisha utekelezaji wa miradi ya maji ya Karatu kwa Tom (kwa gharama ya Shilingi million 623.4, Ayalabe Karatu (Kwa gharama ya shilingi milioni 714.7), pamoja na mradi wa maji wa maeneo ya pembezoni mwa Jiji la Arusha unaofadhiliwa na fedha za UVIKO 19 (kwa gharama ya shilingi milioni 575) miradi yote hiyo inahudumia wananchi kama ilivyokusudiwa.


⦁ AUWSA imefanikiwa kukamilisha utekelezaji wa mradi majisafi wa Namanga, ambao unatokea katika mradi wa majisafi Longido. Kwa sasa inajenga kilomita 145 za mtandao wa kusambaza maji katika mji wa Namanga.


⦁ Vipaumbele vya Mpango na Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023


Ndugu wanahabari,


Ili kuendelea kuboresha huduma na kufikia azma ya Serikali ya kuboresha huduma ya majisafi mijini kufikia asilimia 95, Mamlaka imeweka vipaumbele vifuatavyo katika Bajeti yake ya mwaka 2022/2023.


⦁ Kukamilisha utekelezaji wa mradi mkubwa unaoendelea ili kuongeza hali ya upatikanaji wa majisafi kutoka asilimia 75 ya sasa hadi asilimia 100 ya wakazi wa Jiji la Arusha mwaka 2023.


⦁ Kuendelea kuboresha huduma ya majisafi na usafi wa mazingira katika miji midogo ya Monduli, Ngaramtoni, Usa River na Longido.


⦁ Kutenga fedha kwa ajili ya stahili na madeni ya watumishi.


⦁ Kutenga fedha kwa ajili ya malipo ya watoa huduma mbalimbali wanaoshirikiana na Mamlaka.


⦁ Kuendelea kujiunga na kutumia mifumo mbalimbali ya TEHAMA ya Serikali kwa ajili ya kurahisisha utoaji huduma na kupunguza gharama kwa Serikali.


⦁ Kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya utunzaji wa miundombinu ya majisafi na na usafi wa mazingira.


⦁ Shughuli zitakazotekelezwa kuimarisha huduma:


Ndugu wanahabari,


Kwa Muhtasari, Katika Bajeti ya mwaka wa fedha 2022/2023, Mamlaka imepanga kutekeleza miradi inayogharimu shilingi bilioni 11.8 ya fedha za ndani za Mamlaka ili kuongeza hali ya upatikanaji wa huduma katika eneo lake kama ifuatavyo;


⦁ Kujenga mtandao mpya wa majisafi kwa urefu wa kilomita 215.961 katika maeneo mbalimbali ambayo ni: (Kilomita 90 maeneo ya Kiserian, Moshono, Murieti, Mkonoo, Laizer, Mtoni, Mlangarini, Safari City, Olmoti, Sokoni I na kilomita 36.1 kutoka Olmoti na tanki la Murriet kwenda Bondeni City,) (Kilomita 35.5 mji wa Monduli), (kilomita 13.8 mji wa Usa River), (kilomita 30.561 mji wa Ngaramtoni) na (kilomita 10 mji wa Longido);


⦁ Kuunganisha wateja wapya 13,993 kati ya hao wateja 10,893 katika Jiji la Arusha, na wateja 3,100 miji midogo;


⦁ Kuongeza mtandao wa majitaka kwa kilomita 10 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Arusha;


⦁ Kuunganisha wateja 4,200 katika huduma ya uondoaji wa majitaka;


⦁ Kujenga chemba za kuhifadhia dira za wateja dhidi ya uharibifu na wizi wa dira za maji, ambapo chemba 1,237 zinajengwa ili kuhamishia dira 5000 za wateja wa majumbani;


⦁ Kuboresha mtandao chakavu wa majisafi katika maeneo mbalimbali kwa kilomita 64 jiji la Arusha, na miji midogo kilomita 40.7;


⦁ Kuendelea kutunza vyanzo vya maji vinavyotumika jijini Arusha pamoja na miji midogo;


⦁ Kuendelea na ujenzi wa vyanzo vya maji vya Benett, Komolonike and Lengine Juu Monduli pamoja na kujenga kingio la maji eneo la Mlima Longido.


⦁ Kuendelea na Maboresho ya matanki ya matanki ya kuhifadhia maji (Tanki la Mt. Meru, engikareti na mawili eneo la Longido Mlimani) pamoja na kujenga matanki mapya eneo la Monduli yenye ujazo wa lita 500,000 Mlimani mashariki na lita 300,000 Lengine juu, kujenga tanki la ujazo wa lita 1000,000 na dozing facilities eneo la Momela;  


⦁ Kuanza ujenzi wa ofisi mpya za kanda ya Longido na Monduli ili kuboresha mazingira ya kutolea huduma kwa wananchi;


⦁ Ununuzi wa vitendea kazi (Pikipiki 23 na Bajaji 14); na


⦁ Kufanya maboresho ya majengo ya Ofisi Kuu za sasa pamoja na majengo mengine ya Mamlaka yanayohitaji ukarabati.


⦁ Hitimisho


Ndugu wanahabari,


AUWSA imejipanga kutekeleza miradi ya majisafi kwa ufanisi na kwa wakati ili kuhakikisha wananchi wa Arusha wanapata huduma ya majisafi na salama kwa asilimia 95 mijini kama inavyoelekezwa katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi. 


Aidha, AUWSA inawaasa wananchi wa Arusha kuendelea kutunza miundombinu pamoja na vyanzo vya maji, kuhakiki usomaji wa dira zao pale wanapopokea ujumbe mfupi baada ya usomaji, kulipa ankara kwa wakati, kushiriki katika kusaidia kuzuia wizi wa maji kwa kuwafichua wanaohusika na wizi kupitia namba ya bure ya huduma kwa mteja 0800 110 069.


Mamlaka inatoa shukrani kwa Serikali kupitia Viongozi wa Wizara ya maji kwa miongozo na maelekezo ya kisera inayotoa ili kuboresha utendaji kazi wa Mamlaka za maji Nchini, Pia, Mamlaka inatoa shukrani kwa Uongozi wa Mkoa wa Arusha kwa ushirikiano inaoupata katika kutekeleza shughuli zake za kila siku.


 “SENSA ni Msingi wa Mipango ya Maendeleo; Shiriki kuhesabiwa kwa mustakabali wa maendeleo ya Sekta ya maji na Taifa kwa ujumla”




Naomba kuwasilisha.




Mhandisi Justine G. Rujomba


MKURUGENZI MTENDAJI


MAMLAKA YA MAJISAFI NA USAFI WA MAZINGIRA


JIJI LA ARUSHA

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates