Na Mwandishi wetu
Wataalamu wa UNESCO waliowasili nchini mapema wiki hii kwa ajili ya uthibitishaji upya (Revalidation) wa Hifadhi ya kijiolojia ya "Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark" na kutembelea maeneo mbalimbali ndani na nje ya hifadhi ya Ngorongoro wamehitimisha ziara hiyo leo tarehe 25 Julai, 2024 kwa kufanya kikao cha mwisho (exit meeting) kilichojumuisha menejimenti ya NCAA, mwakilishi wa UNESCO na NATCOM Tanzania pamoja na wawakilishi wa Wilaya za Karatu na Monduli mkoani Arusha.
Wakati wa ziara yao ndani na nje ya hifadhi hiyo ujumbe huo ulitembelea eneo linalojengwa Makumbusho ya Hifadhi ya Kijiolojia ya Ngorongoro-Lengai UNESCO Global Geopark, eneo la nyayo za Laetoli, Makumbusho ya Olduvai, bonde la Olduvai, mchanga unaohama, jamii za makabila ya wairaqw, wahadzabe na wadatoga zinazoishi pembezoni mwa ziwa Eyasi katika wilaya ya Karatu.
Ujumbe huo pia umetembelea shule ya msingi za Tumaini Junior Pre and Primary School na shule ya Father Lieberman Pre and Primary School zilizoko Karatu, kutembelea na kuona shughuli za uwindaji, uhunzi, urithi wa utamaduni na utunzaji wa mazingira zinazofanywa na wanafunzi na makabila yanayozunguka hifadhi ya Ngorongoro ili kuona jinsi hifadhi inavyoshirikisha jamii kusaidia kuhifadhi urithi wa utamaduni wao na mazingira yanayowazunguka.
Aidha, wataalam hao ambao ni wabobezi katika eneo la utalii wa Jiolojia na akiolojia wametembelea Kreta ya Ngorongoro kuona alama mbalimbali za jiopaki pamoja na kutembelea eneo la Laetoli kuangalia tabaka mbalimbali zilizotunza historia ya kidunia kuhusu wanyama na binadamu wa kale duniani walioishi takribani miaka milioni 3.6 iliyopita na kuona jitihada za Serikali kupitia NCAA katika uhifadhi wa urithi huo.
Kamishna wa Uhifadhi wa NCAA Dkt. Elirehema Doriye akiwaaga wataalam hao amewahakikishia kuwa mamlaka hiyo itaendelea kuhifadhi, kulinda, kutangaza na kufuata masharti na miongozo ya UNESCO katika kulinda hadhi ya eneo hilo ili kuendelea kuwa Hifadhi ya Kijiolojia inayotambulika kama “Ngorongoro Lengai UNESCO Global Geopark” ambapo Tanzania ni nchi ya pili Afrika kuwa na hadhi hiyo baada ya nchi ya Moroco.
Maeneo yenye hadhi za Jiolojia (Geopark) za UNESCO zinakaguliwa kwa kina kila baada ya miaka minne kwa ajili ya kupima na kuona ufanisi na ubora wao kupitia shughuli mbalimbali zinazofanyika katika maeneo hayo kwa kufuata vigezo vilivyoainishwa na UNESCO.