MARUFUKU KULIMA, KUINGIZA MIFUGO NDANI YA VYANZO VYA MAJI-MAJALIWA.

 Waziri Mkuu, Kassim Majliwa akisalimiana na Mkurugenzi wa Kampuni ia SAS, Bw. Salim Abri  wakati alipokwenda kwenye shamba la ng'ombe la ASAS lililoko nje kidogo ya mji wa Iringa Januari 19, 2017. (Picha na Ofisi ua Waziri Mkuu)
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akitazama ukamuaji ng'ombe wa maziwa katika shamba la Ng'ombe la ASAS nje kidogo ya mji wa  Iringa Januari 19, 2017.  Wapili kushoto  ni Mkuu wa mkoa wa Iringa, Amina Masenza.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na wakurugenzi wa kampuni ya ASAS  baada ya kutembelea shamba la ng'ombe la ASAS nje kidogo ya mji wa Iringa Januari  19, 2017.   Kulia ni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakuu wa mikoa ya Singida, Mbeya, Iringa na Dodoma wawasimamie wananchi wao na kuhakikisha hakuna shughuli za kibinadamu zinazofanyika ndani ya vyanzo vya maji.

Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Januari 19, 2017) alipozungumza na watumishi wa kituo cha kuzalisha umeme cha Mtera alipotembelea bwawa la Mtera akiwa njiani kwenda mkoani Njombe kwa ziara yake ya kikazi.
Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo baada ya Kaimu Meneja wa Kituo cha kuzalishia umeme cha Mtera, Mhandisi Edmund Seif kutaja baadhi ya changamoto zinazokikabili kituo hicho kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji.
Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu ameagiza vifanyike kwa vikao vya ujirani mwema ili wananchi waelimishwe umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na ni marufuku kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya kilomita 60 kutoka kwenye chanzo.
"Marufuku wafugaji kuingiza ng'ombe ndani ya vyanzo vya maji na badala yake utafutwe utaratibu wa kuwachimbia mabwawa pembeni. Pia wakulima nao wazuiwe kulima ndani ya vyanzo vya maji. Lazima tushirikiane kulinda vyanzo vyetu," amesema.
Awali, Mhandisi Seif alisema kituo hicho cha Mtera kinazalisha megawati 80 kwa siku ambazo zinaingizwa kwenye gridi ya Taifa. Alisema bwawa hili kwa sasa lina maji ya kutosha kuzalisha umeme hadi msimu ujao wa mvua.
Mhandisi hiyo alisema bwawa hilo linategemea kupata maji kutoka mto Ruaha Mkuu, mto Ruaha Mdogo na Vyanzo vyote hivyo vinaathiriwa na shughuli za kibidamu ambapo watu wanalima na kuingiza mifugo.
Baada ya kutoka kituoni hapo Waziri Mkuu alitembelea shamba la Igingilanyi ambalo ni moja kati ya mashamba matatu ya kufugia ng’ombe yanayomilikiwa na kiwanda cha kuzalisha bidhaa za maziwa ya Asas kilichoko mkoani Iringa.
Akiwa shambani hapo Waziri Mkuu aliwaagiza wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanasimamia vizuri mgawanyo wa ardhi ndani ya halmashauri zao pamoja na kusimamia mipaka kati ya wilaya na wilaya.
“Wekeni mipango bora ya matumizi ya ardhi. Pimeni ardhi na mgawe hati ili kumaliza migogoro ya ardhi hata kwa waliopewa mashamba makubwa nao wapimiwe na ardhi yao na wapewe hati kwa mujibu wa muda uliowekwa kisheria,” amesema.

Pia aliwataka Maofisa Mifugo kuongeza kasi ya kutambua mifugo iliyoko kwenye maeneo yao na kuiwekea alama ili kuzuia uhamiaji holela wa mifugo kwa lengo la kuzuia migogoro kati ya wafugaji na wakulima.
Kwa upande wake mmoja wa Wakurugenzi wa kiwanda cha Asas, Bw. Fuad Abri alisema kiwanda hicho kina mashamba matatu yenye jumla ya ekari 2,000 na ng’ombe 1,010 kati ya hao 350 hukamuliwa maziwa na kutoa wastani wa lita 5,000 kwa siku.
Alisema katika mashamba hayo wameajiri wafanyakazi 175 na wamefanikiwa kutumia njia ya uhamilishaji (Artificial Insemination) katika mashamba yote na njia hiyo inawasaidia kuchagua jinsia ya ng’ombe wanayohitaji.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU, 
ALHAMIS, JANUARI 19, 2017.

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

Previous Post Next Post