MFANYABIASHARA wa mjini Loliondo mkoani Arusha, Juda Leminde amegoma
kutii amri ya kuondoka katika shamba la shule la ekari zaidi ya 15,
analodaiwa kupora kinyemela na kudai kuwa shamba hilo ni mali yake na
hababaishwi na mtu yeyote.
Vielelezo vya shamba hilo vinaonesha kuwa ni mali ya Shule ya Msingi
Samunge iliyoko Loliondo na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo alitoa
amri kwa Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka na viongozi wengine
wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya hiyo, kuhakikisha wanamtoa
mfanyabiashara huyo ili shule iendelee na mipango yake katika shamba
hilo.
Akizungumza mbele ya mkuu wa wilaya hiyo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo,
Amani Kasone alisema Leminde amegoma kuondoka na anapata huduma zote za
maji kutoka kwa viongozi wa Mamlaka ya Maji wa Kata ya Samunge.
Kasone alisema pamoja na jitihada zake za kutoa taarifa kwa viongozi
wa vitongoji, kijiji na kata, hakuna jitihada zozote zinazochukuliwa za
kumwondoa mfanyabiashara huyo, licha ya Mkuu wa Mkoa, Gambo, kuagiza
aondolewe.
Alisema binafsi ameshindwa kupata ushirikiano kutoka kwa viongozi wa
serikali waliopo karibu. Alisema mfanyabiashara huyo amekuwa akiwatishia
walimu kwa panga na mshale, wakifuatilia kuondoka katika shamba hilo.
Mkuu wa wilaya, Taka akizungumza katika eneo la shamba hilo
alipotembelea na kuona mazao yaliyolimwa katika shamba hilo na
mfanyabishara huyo, alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na uvamizi wa
namna hiyo haukubaliki kamwe.
Taka alimwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ngorongoro, kumsaka na
kumtia ndani mfanyabiashara huyo kwa kukaidi agizo la mkuu wa mkoa,
lililomtaka kuondoka katika shamba hilo.
Gambo alipokuwa katika ziara ya kikazi katika wilaya hiyo, kuangalia
shughuli za maendeleo, moja ya malalamiko aliyoyakuta ni walimu,
wanafunzi na wananchi wa kata hiyo ya Samunge, kumlalamikia kuwa Leminde
kuwa amepora eneo la shule na walimwomba kutatua tatizo hilo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia