WIZARA ya Maliasili na Utalii imetoa ufafanuzi kuwa, Waziri wa Wizara
hiyo, Profesa Jumanne Maghembe hakutoa leseni za umiliki wa vitalu
vipya, bali ameongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa mujibu wa sheria na
kanuni.
Ufafanuzi huo unatokana na habari iliyoandikwa na gazeti la Raia
Mwema la Januari 25-31 Januari 2017, lililodai kuwa waziri Maghembe
anadaiwa kuongeza muda wa leseni za vitalu vya uwindaji kwa kampuni za
uwindaji wa kitalii kinyume na taratibu.
Taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Katibu Mkuu wa Wizara
hiyo jana, ilieleza kuwa waziri alifanya hayo chini ya Kifungu cha 38
(8) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya mwaka 2009 sambamba
na Kanuni ya 16 ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2015.
“Sheria na Kanuni hiyo inaelezea utaratibu wa kuongeza muda wa
umiliki wa vitalu kwa wale walioomba kuendelea na umiliki wa vitalu vya
awali,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Taarifa hiyo alifafanua kuwa Waziri kabla ya kuongeza muda wa umiliki
wa vitalu, alikaribisha maombi kwa wanaotaka kuongezewa muda huo na
maombi hayo yalipitiwa na Kamati ya Ushauri ya Ugawaji wa Vitalu vya
Uwindaji iliyopo kisheria na iliteuliwa Septemba 2013 na kumshauri
waziri.
Alisema uongezaji wa muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji ulifuata sheria, kanuni na taratibu.
“Hivyo tunawaomba wananchi wapuuze habari hiyo, kwani mwandishi
alikusudia kuupotosha umma kwa kunukuu na kutafsiri vifungu vya Sheria
ya Kuhifadhi Wanyamapori isivyo sahihi”.
“Habari hiyo siyo ya kweli, kwani Waziri hakutoa leseni za umiliki wa
vitalu vipya bali ameongeza muda wa umiliki wa vitalu kwa mujibu wa
Kifungu cha 38 (8) cha Sheria ya Kuhifadhi Wanyamapori Namba 5 ya mwaka
2009 na Kanuni ya 16 ya Kanuni za Uwindaji wa Kitalii za mwaka 2015,”
ilieleza taarifa hiyo.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia