WAFANYABIASHARA wa sungura zaidi ya 20 mkoani Arusha, wameilalamikia
Kampuni ya Mradi wa Sungura ya The Rabbit Bliss Limited ya jijini Arusha
kwa kushindwa kuwalipa madai yao ya zaidi ya Sh milioni 20 baada ya
kuuziwa sungura wa nyama na wafugaji hao.
Wafugaji hao wameeleza kupanda mbegu za sungura hao katika Mradi wa
Ufugaji wa Sungura katika kampuni hiyo yenye ofisi zake Ngaramtoni, nje
kidogo ya Jiji la Arusha, kama ambavyo wamekubaliana kwenye mkataba kwa
lengo la kujipatia fedha baada ya mauzo ya sungura, lakini hali imekuwa
fofauti.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika ofisi hizo jana,
wafanyabiashara hao walijiunga mwaka jana katika kampuni hiyo kwa lengo
la kuiuzia kampuni hiyo kwa makubaliano ya Sh 8,000 kila kilo moja ya
nyama ya sungura na kwamba malipo hufanyika kila baada ya wiki mbili.
Mmoja wa wafugaji hao, Godson Makundi alisema alijiunga ndani ya
mradi huo mwaka jana na kununua majike watano wa sungura pamoja na dume
moja kwa gharama ya Sh 950,000 katika kampuni hiyo na kwenda kuwafuga.
Makundi alieleza kwamba baada ya muda, alizalisha jumla ya sungura 21
aliowawasilisha mbele ya kampuni hiyo kwa lengo ya kupatiwa kiasi cha
fedha, lakini cha ajabu hajalipwa fedha zake mpaka sasa.
“Nilileta jumla ya sungura 21 zenye kilo 55 na niliambiwa baada ya
wiki mbili nitalipwa fedha zangu, lakini cha ajabu hadi sasa sijalipwa
chochote,” alisema Makundi.
Lawrence Mosha alisema alijiunga ndani ya mradi huo mwaka jana na
alinunua na kuuza jumla ya sungura 50 kwa kampuni hiyo kwa kiasi cha Sh
milioni moja, lakini hadi sasa anasotea malipo yake.
Mfugaji mwingine, Joseph Minja alisema alilipia mbegu 57 za sungura
kwa gharama ya Sh milioni tano na kuahidiwa kupatiwa sungura hao, lakini
hadi sasa hajapata chochote.
Akijibu malalamiko hayo kwa njia ya simu, Mkurugenzi wa kampuni hiyo,
Payas Ruben alisema kumekuwa na mabadiliko ya uongozi wa kampuni yao,
ambayo kwa kiasi kikubwa yamechangia kuibua migogoro baina yao na wateja
mbalimbali.
Alisema wakati akikabidhiwa kampuni hiyo, Novemba mwaka jana kutoka
kwa mkurugenzi wa awali ambaye ni raia wa Kenya aliyemtaja kwa jina moja
la Mtuwa, alikuta akaunti ya kampuni hiyo ina Sh milioni mbili pekee,
hivyo kwa sasa wameanza kujipanga upya na watafanya malipo ya
wafanyakazi hao ndani ya miezi mitatu kuanzia sasa.
Alisema baadhi ya wafugaji hao hawana mikataba na kampuni kutokana na baadhi yao kufanya makubaliano na malipo nje na taratibu.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia