PANONE FC YATOLEWA KATIKA MASHINDANO YA SHIRIKISHO LA FA MARA BAADA YA KUCHWAPWA BAO 1-0 NA TIMU YA MADINI


Na Woinde Shizza,Arusha
TIMU ya Madini Sc ya mkoani Arusha imefuzu hatua ya 16 bora katika michuano ya Kombe la la Shirikisho la FA baada ya kufanikiwa kuisambaratisha timu ya Panone ya mkoani Kilimanjaro kwa bao 1-0.


Mchezo huo uliokuwa wa vuta nikuvute baina ya timu hizo mbili ulichezwa katika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini hapa na kumalizika ikiwaacha vijana wa Panone vichwa chini wasiamini macho yao.


Ilikuwa dakika ya 79 mshambuliaji wa Madini Awesu Awesu alipoiandikia timu yake goli la pekee na   lililodumu hadi dakika 90 za mpambano huo,ambapo ni muda mfupi baada ya kocha wa timu hiyo Abdallah Juma kufanya mabadiliko dakika ya 75 kwa kumtoa Rajabu Mwaruko na kumwingiza Awesu.


Timu ya Madini ilicheza pungufu uwanjani baada ya mchezaji wao John Emmanuel  kupewa kadi nyekundu  dakika ya 24 kwa kosa la kumfanyia madhambi mchezaji wa Panone Omary Michael.


Akizungumza baada ya mchezo huo Juma alisema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kuendeleza kupata ushindi hali iliyopelekea kikosi chake kufika hatua ya 16 bora na kuweza kukutana na moja ya timu za ligi kuu katika mchezo utakaofuatia.


“Ninafuraha isiyo na kifani kwa kuweza kuwatoa Panone ambayo ni timu inayoshiriki ligi daraja la kwanza, kwa sasa nitahakikisha nawapa mbinu mpya wachezaji wangu ili tutakapokutana na timu ya ligi kuu tuweze kupata ushindi” alisema Juma.


Kwa upande wa Msemaji wa timu ya Panone Omary Mlekwa alisema kosa moja walilolifanya wachezaji wake ndiyo iliyowaghalimu kupoteza mchezo, hivyo kwa sasa watahakikisha wanaelekeza nguvu zao katika michuano ya ligi daraja la kwanza ili waweze kupata ushindi katika michezo yao.

About Woinde Shizza

Mwandishi , Mjasiriamali na Mbunifu wa Mavazi. Email : woindeshizza@gmail.com , Instagram: woindeshizzablog.