BREAKING NEWS

Wednesday, January 4, 2017

WAZIRI MKUU AAGIZA UMEME WA UHAKIKA KISARAWE II


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuhakikisha eneo la Kisarawe II linakuwa na umeme wa uhakika ili kuwezesha viwanda na wananchi wa eneo hilo kupata nishati hiyo. 
Alitoa agizo hilo jana jioni (Jumanne, Januari 3, 2017) wakati alipotembelea kiwanda cha Milkcom kinachozalisha bidhaa za maziwa na kiwanda cha Watercom kinachozalisha maji vilivyoko katika kata ya Kisarawe ii wilayani Kigamboni akiwa katika ziara yake ya kikazi. 
“Waziri wa Nishati ahakikishe eneo hili linapata umeme wa uhakika ili kuviwezesha viwanda hivi kufanyakazi vizuri jambo litakaloongeza uzalishaji. Pia wananchi wanaoishi katika maeneo haya nao watanufaika na upatikanaji wa nishati hiyo,” alisema. 
Waziri Mkuu alisema amefarijika na jitihada za muwekezaji huyo za kuungamkono mkakati wa Serikali ya awamu ya Tano wa kuifanya Tanzania kujenga uchumi wa viwanda utakaoliwezesha Taifa kufikia uchumi wa kipato cha kati ifikapo mwaka 2025. 
Awali, Msemaji wa Viwanda hivyo, Aboubakar Faraj akisoma taarifa ya viwanda hivyo kwa Waziri Mkuu alisema moja ya changamoto zinazowakabili ni pamoja na upatikanaji wa umeme wa uhakika jambo linasababisha kupanda kwa gharama za uzalishaji. 
“Punde umeme unapokatika tunalazimika kutumia majenereta kwa muda mrefu. Hii husababisha ongezeko la gharama za uzalishaji ambazo huumiza kiwanda kwa sababu haiwezekani kumtwisha mzigo huu mlaji,” alisema. 
Faraji alisema changamoto nyingine ni miundombinu ya barabara ambayo usababisha wateja wengi kushindwa kufika kwenye viwanda hivyo kwa urahisi, hivyo aliiomba Serikali kuwatatulia kero hilo. 
Aliongeza kuwa kwa sasa viwanda hivyo vimeajiri watu zaidi ya 1,800, ambapo alisema endapo Serikali itawahakikishia upatikanaji wa umeme na barabara wataongeza ajira kwa asilimia 25 ifikapo mwaka 2018. 
Mapema Waziri Mkuu alizindua wodi ya wazazi katika Zahanati ya Kisarawe ii iliyojengwa kwa ufadhili wa kampuni ya mafuta ya Oilcom. Wodi hiyo yenye vyumba vitatu itawapunguzia akinamama kusafiri umbali mrefu kutuata huduma hiyo.

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
2 MTAA WA MAGOGONI,
S.  L. P. 3021,

Share this:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia

 
Back To Top
Copyright © 2014 MOUNT KILI NEWS. Designed by OddThemes | Distributed By Gooyaabi Templates