Ticker

6/recent/ticker-posts

DAWA YA MALARIA ISIYO NA KEMIKALI YAGUNDULIWA NA WATAFITI NELSON MANDELA


Kushoto ni mtafiti wa maswala ya tiba kutoka Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela, Dk Daniel Shadrak akielezea juu ya dawa hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Manyara Queen Sendika (katikati), kulia kwake ni Makamu mkuu wa Taasisi Profesa Maulilio Kipanyula na kushoto kwake ni Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Nurdin Babu


Watafiti wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) wamefanikiwa kugundua dawa mpya ya ugonjwa wa malaria isiyo na kemikali ya aina yoyote.

 

Wataalamu hao kwa kushirikiana na watafiti kutoka taasisi zingine za tiba nchini Kenya (KEMR) na Afrika Kusini wamefanikiwa kugundua chanjo hiyo mwishoni mwa mwezi Julai, 2024,  baada ya utafiti wa kina wa miaka mitatu.

Chanjo hiyo ya kwanza ya Ugonjwa wa Malaria kupatikana Afrika, nchini Tanzania imepewa jina la ‘Plasquin’, 

Akizungumza jijini Arusha kwenye maonyesho ya nane nane, kanda ya kaskazini, Mtafiti wa maswala ya tiba kutoka Taasisi ya NM-AIST Dk. Daniel Shadrack amesema kuwa dawa hiyo imepatikana kutokana na utafiti wa kina wa miti shamba inayotumiwa kama tiba ya asili ya ugojwa wa malaria.

“Mara nyingi tiba hii ya asili ilihusisha miti shamba aina tofauti ikiwemo mti wa‘Sindelela Ondorata’ ambapo baada ya utafiti tuligundua kweli ina uwezo mkubwa wa kutibu na kukinga Ugonjwa wa malaria” amesema Dk Daniel na Kuongeza;

“Baada ya kuona hivyo tulianza utafiti wa kuiweka katika viwango vitakavyokubalika kwa njia ya vidoge na sasa ndio tumefanikiwa na tunatarajia itakuwa msaada mkubwa kwa nchi za Afrika katika vita dhidi ya ugonjwa wa malaria” Amesema Dk. Daniel.

Amesema chanjo hiyo ambayo ni miti shamba asilia inatumika kwa dozi ya siku 10 pekee na ina uwezo mkubwa wa kutibu mgonjwa aliyeugua malaria au anaetaka kujikinga dhidi ya malaria.


Amesema kuwa hadi sasa hakuna madhara yoyote yaliyobainika juu ya dawa hiyo kwa watu waliojaribiwa.



Kwa upande wake Makamu Mkuu wa Taasisi ya NM-AIST Profesa Maulilio Kipanyula amesema kuwa baada ya watafiti kufanikiwa kugundua dawa  hiyo ya asilia, wanatarajia kufanya mchakato Ili izalishwe zaidi kwa ajili ya kuanza kutumiwa rasmi.

 "Tunatumai itakuwa ngao njema dhidi ya ugonjwa wa malaria na kuokoa maelfu ya watu na watoto wanaokufa kutokana na ugonjwa huo barani Afrika na dunia kwa ujumla” amesema Profesa Kipanyula.



Akizungumza katika maonyesho hayo, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amewataka watafiti hao kuharakisha mchakato wa uthibitishwaji wa chanjo hiyo kwa ajili ya msaada ya watu wanaougua ugonjwa wa malaria kila mwaka.

 

Wakati chanjo hiyo ikipatikana, nchini Tanzania takwimu zinaonyesha watoto 58 kati ya 1000 walio chini ya umri wa miaka mitano waliugua malaria mwaka 2022 na saba kati yao walifariki, kutoka watoto 161 wa mwaka 2015 na iliyoua watoto 18.

Post a Comment

0 Comments