LOTH LUKUMAY AZINDUA KAMPENI ZA UDIWANI KIRANYI, AAHIDI KUTATUA KERO ZA WANANCHI
Mgombea udiwani wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata ya Kiranyi, Elias Loth Lukumay, amezindua rasmi kampeni zake kwa kueleza vipaumbele vyake ambavyo vitasaidia kubadilisha maisha ya wananchi wa kata hiyo endapo atachaguliwa.
Akizungumza katika mkutano wa uzinduzi, Lukumay alisema kero kubwa zinazowakabili wakazi wa Kiranyi ni barabara mbovu, jambo linalosababisha adha kubwa hasa kwa wanafunzi, wagonjwa na wakulima wanaosafirisha mazao yao.
Alibainisha kuwa, iwapo atapewa ridhaa ya wananchi, atashirikiana na serikali kuhakikisha barabara hizo zinakarabatiwa na kupitika wakati wote.
Vilevile, aliahidi kushughulikia changamoto ya huduma ya maji ambayo yamekuwa yakikatika mara kwa mara, hali inayowalazimu wananchi kufuata maji mbali na kutumia muda mwingi unaoweza kutumika kwenye shughuli za maendeleo.
Aidha, Lukumay alisema atajitahidi kuimarisha huduma za kijamii katika kata hiyo ikiwemo afya na elimu, akieleza dhamira yake ya kushirikiana na serikali na wadau mbalimbali kuhakikisha shule zinakuwa na mazingira bora ya kujifunzia pamoja na kuimarisha upatikanaji wa dawa na huduma bora kwenye zahanati.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Arumeru, Noel Severe, aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu, na kuchagua “mafiga matatu” yaani Rais wa CCM, Mbunge na Madiwani.
Alisema kuchagua wagombea wa CCM katika nafasi hizo ni hatua ya kuimarisha mshikamano wa chama na kupeleka maendeleo ya kweli kwa wananchi.
“Kura ni silaha ya mwananchi Ni haki na wajibu wa kila mmoja, hivyo ni vyema kila mkazi akajitokeza na kushiriki kikamilifu,” alisema Severe.
Aidha, aliwahimiza wananchi kuendeleza amani na mshikamano kipindi chote cha kampeni, akisisitiza kuwa uchaguzi ni sehemu ya mchakato wa demokrasia na chanzo cha vurugu.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia