TUISHIME SCHOOL YAFANYA MAHAFALI YA 15, MKURUGENZI ATOA WITO WA MALEZI BORA KWA WATOTO
Na Mwandishi Wetu, Arusha
Shule ya Tuishime imefanya mahafali yake ya 15 ya darasa la saba, ambapo jumla ya wanafunzi 26 wamehitimu masomo yao kwa mwaka huu wa 2025.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na wazazi, walimu na wadau wa elimu waliokuja kusherehekea mafanikio ya watoto wao.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Shule ya Tuishime Naomi Masenge alisema shule hiyo imekuwa ikitoa elimu bora na malezi ya maadili ili kuwaandaa wanafunzi kuwa raia wenye mchango chanya kwa jamii.
“Lengo letu si kuwafundisha watoto kusoma na kuandika pekee, bali tunataka tuwajenge kiakili, kimwili na kimaadili ili wawe viongozi wa kesho wenye heshima na nidhamu,” alisema Mkurugenzi.
Aidha, aliwataka wazazi kuendelea kushirikiana na walimu kwa kuhakikisha watoto wanapata malezi mema hata wakiwa majumbani.
Alisema wazazi ndio msingi wa nidhamu na maadili ya mtoto, na shule huendeleza kile kinachojengwa nyumbani.
“Tunawaomba wazazi msipuuze malezi ya watoto ,Msipowajenga vizuri, mitaa itawajenga vibaya ,elimu nzuri huanzia nyumbani na shule huchangia kumalizia,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, aliwapongeza wanafunzi waliomaliza darasa la saba kwa bidii na nidhamu waliyoonyesha kipindi chote cha masomo ,huku alibainisha kuwa kuwa shule itaendelea kushirikiana na jamii kuhakikisha wanafunzi wanapata malezi bora.
“Wanafunzi hawa wamepata msingi imara wa elimu na maadili. Tunawaamini wataendelea kuonyesha nidhamu njema katika shule za sekondari na hata baadaye maishani,” alisema Mwalimu Masenge.
Mahafali hayo yaliambatana na burudani mbalimbali zikiwemo ngoma, mashairi na nyimbo zilizotungwa na wanafunzi, zikionyesha furaha ya kumaliza elimu ya msingi na shukrani kwa walimu wao.

0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia