COSTECH YAKUTANA NA WAFADHILI KUJADILI UTEKELEZAJI WA PROGRAMU YA UTAFITI YA U’GOOD!?
TUME
ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) imekutana na wasimamizi na wafadhili
wa programu ya utafiti ya u’Good!? kujadili utekelezaji wa programu
mbalimbali za utafiti zinazolenga kuleta matokeo chanya kwa jamii,
hususan katika kuchochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Mkutano
huo umefanyika leo Oktoba 7, 2025, Dar es Salaam ukihusisha wafadhili
kutoka Baraza la Utafiti la Afrika Kusini (NRF) na Shirika la BOTNAR la
Uswisi, lengo likiwa ni kujenga jamii yenye ustawi hususani kwa vijana.
Programu
hiyo inahusisha watafiti kutoka nchi 9 za ukanda wa kusini mwa Jangwa
la Sahara, Asia, Ulaya, na Amerika Kusini, ambao ni wanufaika wa mradi
huo unaolenga kuchochea ustawi wa vijana na jamii kwa ujumla kupitia
tafiti za kijamii na kiuchumi.
Akizungumza
katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Utafiti wa Tume ya Sayansi na
Teknolojia (COSTECH), Dkt. Bugwesa Katale, amesema Tanzania ni miongoni
mwa wanufaika wa mradi huo kupitia ushiriki wake katika umoja wa mipango
ya ruzuku za kisayansi unaoundwa na wanachama 17.
“COSTECH
ilituma maandiko 120, ambapo 23 kati ya hayo yalishinda na kusaidia
nchi kupata jumla ya miradi tisa itakayotekelezwa kwa ushirikiano na
watafiti kutoka nchi tisa tofauti,” amesema Dkt. Katale.
Aidha,
ameongeza kuwa programu hiyo ni muhimu kwa kuwa inaleta pamoja watafiti
kutoka mataifa mbalimbali kufanya tafiti zitakazochochea hali bora ya
maisha na ukuaji wa uchumi wa wananchi.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi wa Maarifa na Mitandao ya Kitaasisi wa NRF
Afrika Kusini, Dkt. Dorothy Ngila, amesema lengo kuu la mradi huo ni
kuhakikisha bara la Afrika linapata nafasi ya kutoa sauti zake katika
majukwaa ya kimataifa kuhusu jinsi ya kuzalisha maarifa mapya na
kuunganisha vijana kupitia tafiti za pamoja.
“Tunataka
bara la Afrika liwe na sauti moja kimataifa katika kutengeneza maarifa
na mbinu bora za kusaidia vijana kustawi,” amesema Dkt. Ngila.
Naye
Profesa Sharlene Swartz kutoka Human Sciences Research Council (HSRC)
ya Afrika Kusini amesema wameamua kufadhili miradi 23 tofauti inayolenga
kuchunguza uhusiano wa kijamii kati ya vijana na namna bora ya kujenga
ustawi wa pamoja.
“Tunataka
kuona vijana wanatumia tafiti hizi kuimarisha mshikamano na ustawi wa
kijamii, si mafanikio ya mtu mmoja mmoja,” amesema Profesa Swartz.
Kwa
upande wake, Dkt. Victoria Mwakalinga kutoka Chuo Kikuu cha Ardhi
amesema utafiti huo utakuwa na mchango mkubwa katika utekelezaji wa sera
mbalimbali, hususan zinazohusu maendeleo ya vijana wanaoishi vijijini,
kwa kuangalia mbinu bora za uzalishaji wa mazao katika mazingira
yanayokabiliwa na mabadiliko ya tabianchi.
Mkutano
huo ambao umezinduliwa rasmi leo Oktoba 6, 2025, unatarajiwa kufungwa
Oktoba 9, 2025, ukiwa na kaulimbiu isemayo: “Kustawi Pamoja, Ustawi wa
Uhusiano wa Vijana kwa Mustakabali wa Kimataifa wa Kusini mwa Dunia.”





0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia