ELIMU YA WATU WAZIMA YAZIDI KUPAA ARUSHA
Mgeni Rasmi katika hafla ya maadhimisho ya wiki ya Elimu ya Watu Wazima Wilaya ya Arusha,Bi. Chausiku Baha akivalishwa skafu na mmoja wa Wanafunzi waliopata elimu nje ya mfumo rasmi.
Na Woinde Shizza, Arusha
Mamamia ya wananchi, walimu, wanafunzi na wadau wa elimu wamejitokeza leo kushiriki maadhimisho ya Wiki ya Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Levolosi, jijini Arusha.
Maadhimisho hayo, yaliyopewa kauli mbiu “Elimu Endelevu kwa Maendeleo ya Jamii”, yamelenga kuhamasisha jamii kuhusu nafasi ya elimu kwa kila Mtanzania bila kujali umri au changamoto zilizomkumba awali.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Arusha Mjini, Afisa Tarafa wa Levolosi, Chausiku Baha alisema serikali imeweka mikakati ya kuhakikisha wananchi wote wanapata elimu bora na stadi za maisha zitakazowasaidia kuboresha maisha yao.
“Elimu ya watu wazima imekuwa kichocheo cha maendeleo ya kijamii na kiuchumi ,tunawahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki programu hizi,” alisema Chausiku.
Wadau wa elimu walioshiriki walieleza kuwa elimu nje ya mfumo rasmi ni nyenzo muhimu katika kupunguza ujinga, kuongeza maarifa ya kijamii na kuimarisha stadi za maisha kwa wananchi waliokosa fursa ya elimu ya msingi.
Mmoja wa wanafunzi wa elimu ya watu wazima, Margareth Daudi, alisema elimu hiyo imemwezesha kuboresha maisha yake kwa kujua kusoma, kuandika na kufanya biashara kwa ufanisi.
“Nilianza bila kujua kusaini jina langu, sasa nasoma mikataba na kupanga bei za bidhaa zangu,” alisema kwa furaha.
Kwa upande wake mkufunzi mkazi kutoka taasisi ya elimu ya watu wazima Mwl. Aminiel Vavayo alisema mwamko wa wananchi kujitokeza kujifunza umeongezeka na unachangia kupunguza utegemezi na kuongeza ubunifu katika jamii.
“Tunawaona wanafunzi wakibadilika kimaisha Wengine wamefungua miradi, wengine wamejiunga na vikundi vya kifedha Hii ni ishara kwamba elimu hii ina tija,” alisema.
Kwa upande wake afisa elimu ya watu wazima mkoa wa Arusha Emmanuel Mahondo alisema kuwa mpakasasa jumla ya wasichana 249 wanaendelea kunufaika na mfumo Katika mkoa wa Arusha na wanajumla ya vituo 12 vinavyotoa huduma Katika mkoa mzima
"Nichukuwe Tu kuwaambia wazazi kuwa wasiwafiche watoto ndani kisa wamekati masomo kwa sababu labda ya kupata mimba za utoto ,au changamoto yoyote Ile badala yake wawatoe watoto waende mashuleni kujifunza na ndio maana mama Samia aliamia kuja na mfumo hii WA elimu ya watu wazima" alisema
“Najivunia kuona wanafunzi wangu wanapata maarifa na kujipambanua ,Natoa wito kwa jamii kujiunga na elimu ya watu wazima inayotolewa bila malipo,” amesema Mwalimu Amina.
Kwa upande wake, mnufaika wa elimu hiyo, Oliva Shayo (46), amesema anajivunia kuondokana na utegemezi baada ya kupata ujuzi wa kushona nguo, ambao umemwezesha kujitegemea kiuchumi.
“Niliianza masomo mwaka 2017 nikiwa na watoto watano. Nilijituma na kufanikiwa kupata ujuzi wa ushonaji, jambo lililonisaidia kununua mashamba na kujipatia kipato cha kutosha. Nawasihi wanawake wenzangu waache woga, waje wapate maarifa ili kuondoa ujinga na kusukuma gurudumu la maendeleo ya maisha yao,” amesema Oliva.
Naye Songo Meere, mmoja wa wanufaika wa elimu hiyo katika kituo cha MUKEJA, ameshukuru hatua aliyofikia ya kujua kusoma na kuandika. Amesema ana mpango wa kuendelea kuhamasisha vijana wa jamii ya Kimasai ambao bado hawajui kusoma na kuandika, ili nao waweze kunufaika na fursa hiyo




0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia