VYAMA VYA USHIRIKA WA AKIBA NA MIKOPO VYASISITIZWA KUZINGATIA SHERIA NA MIONGOZO
Na Woinde Shizza, Arusha
Vyama vya ushirika wa akiba na mikopo (Saccos) nchini vimetakiwa kuzingatia misingi, taratibu, sera na miongozo inayotolewa na serikali kwa lengo la kuondoa migogoro inayoweza kuathiri ukuaji wake na kuhakikisha maendeleo ya jumuiya yanapatikana kwa wakati.
Wito huo umetolewa katika maadhimisho ya Siku ya Ushirika wa Akiba na Mikopo Tanzania yaliyofanyika mwaka huu, yakilenga kujadili njia madhubuti za kushughulikia changamoto zinazoikumba sekta hiyo na kupata miongozo bora itakayowezesha kuimarisha uchumi wa wanachama.
Mwenyekiti wa vyama vya kifedha (Sccult), Ernest Nyambo, alisema ushirika unasonga mbele kwa kasi na umeendelea kuwa chachu ya kufanikisha malengo ya kiuchumi kwa wananchi wa kipato cha chini.
“Teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA) imekuwa changamoto, lakini tumeendelea kuwaelimisha wanachama namna bora ya kuitumia na faida zinazopatikanaMwaka huu tumeshuhudia wanachama zaidi ya 900 wakihudhuria, idadi ambayo ni mara dufu ya mwaka jana,” alisema Nyambo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Tanzania Bara, Usekelege Mpula, alisema migogoro ya kazi ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha ustawi wa vyama hivyo, na kusisitiza kuwepo kwa sheria madhubuti zitakazosaidia kumaliza migogoro kwa ufanisi.
Naye Mwanadiplomasia Mwandamizi na mbobezi wa masuala ya uongozi wa kimkakati, Omary Mjenga, alibainisha kuwa ukosefu wa uwazi na kutoweka mambo bayana ndio chanzo kikuu cha kudidimia kwa vyama vya ushirika.
“Uongozi sio cheo, bali ni jukumu la kuhakikisha wanachama wananufaika. Ni vyema kuongoza kwa malengo, ili wanachama waone faida ya kuwa sehemu ya Saccos. Tukifanya hivyo sasa, miaka mitano ijayo vyama hivi vitakuwa mbali zaidi,” alisema.
Mshiriki wa maadhimisho hayo, Edius Langoga, aliiomba serikali kuendelea kuweka sera na sheria rafiki zitakazowezesha taasisi hizo kutimiza malengo yao na kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wanachama zaidi ya 900 kutoka vyama mbalimbali vya ushirika nchini, yakionesha mshikamano na dhamira ya pamoja ya kuendeleza ukuaji wa sekta ya ushirika wa kifedha Tanzania.
.jpg)

0 Comments:
إرسال تعليق
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia