EQUITY BANK YAAHIDI KUENDELEA KUWEKEZA KATIKA MFUMO WA KIDIGITALI NA ELIMU YA FEDHA
Benki ya Equity Tanzania imeahidi
kuendelea kuwekeza katika mifumo ya kidigitali, kupanua matawi na
kuongeza elimu ya fedha kwa wananchi, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za
kukuza ujumuishaji wa huduma za kifedha nchini.
Akizungumza leo
jijini Dar es Salaam wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja,
Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Bi. Isabella Maganga, alisema Equity
inaendelea kuimarisha ubunifu ili kuhakikisha Watanzania wanapata
huduma bora, nafuu na salama zaidi kupitia njia za kidigitali na matawi
mapya yatakayofunguliwa katika maeneo mbalimbali ya nchi.
“Kaulimbiu
ya mwaka huu, ‘Mission is Possible’, inaakisi dhamira yetu ya
kuwawezesha wateja kufikia mafanikio ya kifedha na kibiashara.
Tumeendelea kukuza ujumuishaji wa kifedha kupitia bidhaa rafiki zisizo
na makato makubwa, zinazomwezesha Mtanzania wa kipato cha chini kupata
huduma za kibenki kwa urahisi zaidi,” alisema Maganga.
Kwa
upande wake, Bw. Prosper Nambaya, Mkurugenzi wa Biashara wa Equity Bank
Tanzania, alisema benki hiyo inaendelea kupanua mtandao wake wa huduma
kwa kuongeza matawi mapya, kuimarisha huduma za internet banking, na
kuongeza idadi ya mawakala wa kibenki hadi kufikia zaidi ya 3,000 nchi
nzima.
Aliongeza kuwa, hadi kufikia mwaka 2030, benki hiyo
inalenga kuwa na matawi 55 pamoja na ushirikiano mpya kupitia Umoja
Switch utakaowawezesha wateja kutumia zaidi ya ATM 1,000 kote nchini.
Wakati huo huo, baadhi ya wateja wa benki hiyo wameelezea kuridhishwa kwao na huduma za Equity.
Uinde Muro, Mkurugenzi wa Imperium OpEx, alisema benki hiyo imemsaidia
kukua kibiashara kupitia huduma zinazojali mahitaji ya mteja.
Naye Benson Maenya, Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya GSM, alisema
Equity imekuwa mshirika muhimu katika kupanua biashara zake ndani ya
ukanda wa Afrika Mashariki kutokana na mtandao wake mpana wa kimataifa
na huduma bora kwa wateja.



0 Comments:
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia