NYAHIRI YAJIPAMBANUA KUWA KINARA WA ELIMU BORA ARUSHA




Na Woinde Shizza , Arusha 

Shule ya Sekondari Nyahiri imeendelea kung’ara katika utoaji wa elimu bora mkoani Arusha, baada ya kuendesha mahafali ya darasa la saba na kidato cha nne kwa mbwembwe, shangwe na hamasa kubwa huku ikitaja mikakati kabambe ya kuinua kiwango cha elimu na ubunifu kwa wanafunzi wake.

Akizungumza katika hafla hiyo iliyofanyika shuleni  apo Mkurugenzi wa shule hiyo, Michael Kimbaki, alisema Nyahiri imejipambanua kama taasisi kinara katika kutoa elimu bora yenye matokeo chanya, huku ikileta mapinduzi katika malezi ya wanafunzi wenye nidhamu, ujasiri na uwezo wa kujitegemea.



“Tumejenga mfumo wa kuwafanya wanafunzi wetu wawe wabunifu, wachapakazi na wanaojiamini. Tunawafundisha kufikiri kwa kina na kubuni majibu yao kwa uelewa mpana, badala ya kukopi na kupesti,” alisema Kimbaki.

Aidha, Kimbaki alifichua kuwa shule hiyo imeanzisha mpango maalum wa ufadhili wa masomo nje ya nchi (Scholarship) kwa wanafunzi wanaofanya vizuri zaidi, kama njia ya kuwahamasisha kujituma.

“Baada ya kubaini changamoto ya ushindani wa ajira duniani, tumeanzisha program ya scholarship kwa wanafunzi wanaong’ara. Hadi sasa, wanafunzi watatu wananufaika na ufadhili huo na wanasoma nchini China, Uingereza na Uturuki,” aliongeza kwa fahari.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo alitangaza mipango ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa jengo la utawala la kisasa lenye ukumbi wa mikutano, bwalo la chakula na maktaba ya kisasa, vitakavyowawezesha wanafunzi kujisomea kwa ufanisi zaidi.

“Tunahitaji Nyahiri iwe mfano wa shule bora si Arusha pekee bali Tanzania kwa ujumla. Tunajenga miundombinu itakayowasaidia watoto wetu kusoma katika mazingira bora, yenye ubunifu na utafiti,” alisema.

Kwa upande wake, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Petro Mwita, aliwapongeza wahitimu kwa bidii na nidhamu waliyoionyesha kipindi chote cha masomo yao, huku akiwashukuru wazazi na walimu kwa ushirikiano mkubwa uliowezesha mafanikio hayo.


“Tunajivunia kuona wanafunzi wetu wakifikia hatua hii muhimu. Safari ya elimu si rahisi, inahitaji kujituma na kujitambua. Nyahiri imekuwa kitovu cha malezi bora ya kielimu na kimaadili,” alisema Mwita.

Aidha, aliwahimiza wazazi kuendelea kushirikiana na walimu katika kulea watoto katika misingi ya heshima, bidii na upendo wa kujifunza.

“Elimu ni urithi wa kudumu. Wazazi msichoke kuwekeza katika elimu ya watoto wenu, kwani hiyo ndiyo njia pekee ya kuwafungulia milango ya mafanikio,” alisisitiza Mwita.

Hafla hiyo ilihusisha burudani mbalimbali zikiwemo nyimbo, michezo na maonesho ya vipaji vya wanafunzi, ikiashiria furaha na mafanikio ya shule hiyo ambayo imekuwa ikionyesha maendeleo ya haraka katika ubora wa elimu na malezi.


About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia