WIKI YA HUDUMA KWA WATEJA: EWURA YAWA KARIBU ZAIDI NA JAMII

 





Na Woinde Shizza, Arusha

Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) Kanda ya Kaskazini imeadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja kwa kuendelea kusogeza huduma karibu na wananchi, hatua inayolenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu haki, wajibu na matumizi sahihi ya nishati na maji.

Tukio hilo limefanyika jijini Arusha likihusisha maofisa wa EWURA, wadau wa sekta za nishati na maji pamoja na wananchi waliojitokeza kupata elimu, kutoa maoni na kuuliza maswali kuhusu huduma mbalimbali zinazodhibitiwa na mamlaka hiyo.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, Meneja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Lorivii Long’idu, alisema wiki ya huduma kwa wateja ni jukwaa muhimu linalowapa wananchi nafasi ya kuelewa kazi za EWURA, kutoa maoni yao na kushiriki katika maboresho ya huduma zinazotolewa.

“Tunataka wananchi watambue kwamba EWURA ipo kwa ajili yao, huduma bora haziwezi kupatikana bila ushirikiano kati ya wateja na watoa huduma,” alisema Long’idu.

Aliongeza kuwa, mbali na kutoa elimu kwa wananchi, EWURA pia imeendelea kuboresha mifumo yake ya kiutendaji ikiwemo kuanzisha mfumo wa utoaji leseni mtandaoni unaowezesha waombaji kupata vibali kwa urahisi bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.



Kwa upande wake, Afisa Huduma kwa Wateja wa EWURA Kanda ya Kaskazini, Bahati Tibakunda, alisema mamlaka hiyo imejipanga kuendelea kutoa elimu ya mara kwa mara kuhusu matumizi sahihi ya gesi, mafuta na maji, sambamba na kupokea maoni kutoka kwa watumiaji.

“Tumeona umuhimu wa kutoa elimu ya moja kwa moja kwa wananchi ili waweze kuelewa haki zao, wajibu wao, na namna bora ya kutoa taarifa pale wanapokumbana na huduma zisizo na ubora,” alisema Tibakunda.


 

Baadhi ya wananchi walioshiriki maadhimisho hayo waliipongeza EWURA kwa kuandaa kampeni hiyo wakisema imekuwa msaada mkubwa katika kuwajengea uelewa kuhusu masuala ya ubora wa huduma, usalama na haki za watumiaji.

Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa kila mwaka nchini kwa taasisi za umma na binafsi, ikilenga kuimarisha mahusiano kati ya watoa huduma na wateja wao, sambamba na kujenga utamaduni wa uwazi, uwajibikaji na utoaji wa huduma bora.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia