WANAFUNZI ZAIDI YA 60 WA GLISTEN PRE & PRIMARY SCHOOL WAHITIMU, MILYA ASISITIZA KUISHIKA ELIMU

 


Na Woinde Shizza, Manyara

Shule ya Glisten Pre and Primary School iliyopo Mererani, mkoani Manyara, imefanya mahafali yake ya tano ya darasa la saba ambapo jumla ya wanafunzi 62 wamehitimu, huku viongozi wa shule, wazazi na wageni waalikwa wakisisitiza umuhimu wa elimu bora kama nguzo ya maendeleo ya taifa.

Akisoma hotuba kwa niaba ya Mkurugenzi wa shule hiyo, Mwalimu wa Taaluma Athanas Christopher alisema shule hiyo imeendelea kutoa elimu bora inayojenga misingi ya maadili, nidhamu na ubunifu, jambo linaloonekana kwa mafanikio ya wanafunzi wanaoendelea katika shule za vipaji maalumu.

“Tumewaandaa vyema wanafunzi wetu kitaaluma na kimaadili Tunaamini elimu tuliyowapatia itakuwa mwongozo wao katika maisha na kuwasaidia kufikia mafanikio makubwa,” alisema Mwalimu Athanas.



Kwa upande wake, Meneja wa shule hiyo, Justice Nyari, alisema mafanikio hayo yamechangiwa na ushirikiano mkubwa kati ya wazazi, walimu na wanafunzi, pamoja na mazingira bora ya kujifunzia yaliyowekwa na uongozi wa shule hiyo.

“Tunashukuru wazazi kwa kuendelea kuiamini taasisi yetu Tumekuwa tukifanya kazi kwa bidii kuhakikisha kila mtoto anapata elimu yenye ubora, nidhamu na malezi mema ,Mafanikio haya ni matokeo ya ushirikiano wetu,” alisema Nyari.

Mgeni rasmi wa mahafali hayo, ambaye pia ni mgombea ubunge wa Jimbo la Simanjiro, Jemsi Ole Milya, alipongeza shule hiyo kwa juhudi kubwa katika kuendeleza elimu na kuwataka wanafunzi kuishika elimu kama silaha ya mafanikio katika maisha.

“Elimu ni urithi bora kuliko mali yoyote, Nawasihi watoto wetu waishike elimu, wasome kwa bidii na kuendelea kuwa na nidhamu, Elimu itawafungua milango ya mafanikio makubwa,” alisema Milya.



Milya alisisitiza kuwa wazazi wanapaswa kuendelea kuwahimiza watoto kusoma licha ya changamoto za kifamilia au kiuchumi, akitahadharisha kuwa kuacha kumsomesha mtoto ni sawa na kumnyima maisha bora.

“Kama mzazi akikosa ada, asikate tamaa, Ni bora akauza hata mali ndogo alizonazo ili mtoto aende shule ,elimu ndiyo msingi wa maisha bora,” aliongeza.

Kadhalika, alihimiza Watanzania kuendelea kuienzi amani, kuipenda nchi na kumheshimu Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendeleza juhudi za kuinua sekta ya elimu nchini.

“Tuilinde amani ya nchi yetu, tukipoteza amani, tutapoteza kila kitu, Tumpende Rais wetu na tuiombee nchi yetu iendelee kuwa na utulivu,” alisema kwa msisitizo.

Naye mzazi rasmi wa mahafali hayo, Dhulfa Laizer, alipongeza walimu na uongozi wa shule hiyo kwa malezi bora wanayowapa wanafunzi, akibainisha kuwa shule hiyo imekuwa zaidi ya taasisi ya elimu, bali ni chimbuko la maadili mema.

“Walimu wa Glisten wamekuwa zaidi ya wazazi kwa watoto wetu Hapa mtoto analelewa, anafundishwa na kuandaliwa kwa maisha ya baadaye.,tunawashukuru kwa kujitoa kwao,” alisema Dhulfa.

Kwa upande wake, mwanafunzi bora wa shule hiyo Jamillar khalid, Alishukuru wazazi, walimu na uongozi wa shule kwa mchango wao mkubwa katika kufanikisha safari yao ya elimu ya msingi.

“Tumejifunza mengi katika shule yetu ,nidhamu, heshima na kujituma ,tunaahidi kuendelea kuishika elimu na kuitumia vizuri ili kufikia ndoto zetu," alisema mwanafunzi huyo kwa niaba ya wenzake.

Mkurugenzi wa shule hiyo , Justine Nyari, alisisitiza kuwa Watanzania wanapaswa kumpa Rais Samia Suluhu Hassan fadhila kwa kumpa kura nyingi katika uchaguzi wa Oktoba 29 

Alibainisha kuwa taifa halina cha kumlipa Rais isipokuwa kumpa kura zake na kumwombea afya njema na amani, ili mipango mizuri aliyopanga kwa kipindi cha miaka mitano ijayo ikamilike bila vikwazo.

Mahafali hayo yalipambwa na burudani mbalimbali za wanafunzi zenye maudhui ya uzalendo na elimu, ikiwa ni pamoja na ngoma za asili, nyimbo, michezo ya kuigiza na mashairi yaliyobeba jumbe za hamasa kwa wazazi na jamii kuwekeza katika elimu.

About Woinde Shizza

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.

0 Comments:

Post a Comment

unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia