MAHAKAMA ya Haki ya Afrika Mashariki, (EACJ) imetimiza
miaka 10 tangu ilipozinduliwa na kuanza kazi Novemba 2001, ikijivunia kujenga
misingi na kanuni licha ya kuwepo kwa changamoto kadhaa mbele yake. SIKIA MANENO ya Msajili wa mahakama hiyo, Dk. John Luhangisa, kama ifuatavyo.
Swali: Mahakama yako ina umri wa miaka 10 sasa, je,
unaridhika na utendaji wake?
Jibu: Binafsi
ninaridhika na utendaji wa mahakam hii pamoja na majaji na wafanyakazi wake.
Majaji na wafanyakazi wana moyo wa kujituma na hii inajionyesha kwa jinsi
wanavyofanyakazi hadi zaidi ya muda uliopangwa. Mathalan, wengi hufanya kazi
hadi saa 2 za usiku ingawa muda rasmi wa kumaliza kazi ni saa 11 jioni. Majaji
wakija hapa hawana siku za sikukuu au Jumapili, wanachapa kazi muda wote.
Swali: Hii mahakama ina wafanyakazi na majaji wangapi
na wanapataje nafasi hiyo?
Jibu:
Mahakama inao majaji 10, na wote huteuliwa na Mkutano wa Wakuu wa nchi tano
husika. Wafanyakazi wengine wapo 20 ambao walipata nafasi zao baada ya kutuma
maombi ya kazi.
Swali: Mahakama hii ina tofauti gani na mahakama
zingine?
Jibu: EACJ
inasikiliza kesi za madai tu, tofauti na mahakama zingine ambazo husikiliza pia
kesi za jinai. Pili, mtu ye yote akihitaji kufungua kesi hapa, hahitaji kwanza
kupata kibali sehemu yo yote. Na tena mtu ye yote anaweza kufungua kesi dhidi
ya nchi nyingine mwanachama kama imekiuka
makubaliano yake (mkataba wa Jumuiya), basi anawza kufungua kesi dhidi ya nchi
hiyo. Kwa mfano, shirika moja lisilo la kiserikali la Kenya, Africa Network for
Animal Welfare (ANAW) limefungua kesi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya
Muungano ya Tanzania, likipinga azma yake ya kujenga barabara kupita Mbuga ya
Wanyamapori ya Serengeti kwa maelezo kuwa azma hiyo ni uvunjifu wa sheria na ni
ukiukwaji wa kanuni za Mkataba wa Jumuiya ya Afrika Mashariki
Swali:
Baada ya uhai wa miaka 10 ya mahakama yako, imepata mafanikio gani?
Jibu: Mafanikio yamekuwa mengi. Kwanza
imeweza kujenga misingi ambayo walalamikaji au mtu ye yote yule ambaye
angependa kuleta kesi yake mahakamani hapa ataitumia. Yaani, mahakama
imetengeneza kanuni za uendeshaji wa kesi za hapa na hii ni dira muhimu sana.
Pia
imesimama kama taasisi inayojitegemea na yenye
kutoa haki bila woga wala upendeleo, mfano halisi ni maamuzi ya kesi
zilizofanywa imeonyesha kuwa ni taasisi ambayo imejijenga kuwahudumia watu bila
woga na chuki.
Misingi mingine ni uwezo wa
kutumiwa na mtu ye yote yule na hii unakuta katika kanuni zake ambazo hutoa
nafasi kwa mtu ye yote bila kujali uwezo wake kufungua kesi katika mahakama
hii. Na kwa upande wa mtu asiye na uwezo, mahakama inatoa nafasi kwa mtu huyo
baada ya kujiridhisha kwamba ni kweli hana uwezo, kufungua kesi bila kutozwa
gharama. Gharama ya kufungua kesi ni dola za Marekani 500 au chini ya hapo.
Swali: Unaweza kueleza changamoto ambazo inakabiliwa
nazo?
Jibu: Kuna
tatizo la uhaba wa majaji wa kusikiliza kesi. Majaji wanaosikiliza kesi katika
mahakama hii hawakai hapa makao makuu ya EACJ Arusha, bali katika nchi zao
husika. Wanakuja pale hitaji linapotokea, hivyo ni ngumu kuwapangia kazi za
hapa. Sasa Baraza la Mawaziri linatakiwa kuamua majaji wakae hapa muda wote na
hiyo inaweza kuendesha kesi na kumaliza kwa wakati muafaka. Suala la
wafanyakazi pia ni tatizo kwani hawapo wa kutosha kulingana na kazi zilizopo.
Swali: Kuna uwezekano wa EACJ kupanua wigo wa utendaji
kazi zake?
Jibu: Kuongeza
wigo ni suala la wananchi wenyewe, wote wanataka wigo wa mahakama hii
upanuliwe, yaani, iwe ya rufaa. Iweze pia kusikiliza kesi zinazotoka mahakama
kuu au mahakama za rufani za nchi husika. Huo ndio wito wao na hayo ndiyo maoni
ya wananchi.
Bahati nzuri kwa mujibu wa
mkataba, EACJ baadaye itakuwa na uwezo wa kusikiliza kesi za rufaa.
Pia EACJ itakuwa na madaraka
ya kusikiliza kesi zinazohusu haki ya binadamu, lakini mpaka sasa mkataba
haujatengenezwa. Kwa sasa Mahakama ya Haki za Binadamu ya Afrika ndiyo yenye
madaraka hayo.
Swali: Ni kesi ngapi hadi sasa zimekwishamuliwa na
zilikuwa zinahusu nini hasa?
Jibu: Kwa
mara ya kwanza mahakama ilipokea kesi Desemba 2005, iliyofunguliwa na wajumbe
wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kuhusu uchaguzi wa wabunge wa bunge hilo. Kesi hii ilikuwa ya Kenya, ambapo waliofungua walipiga uteuzi wa
wabunge katika bunge hilo
badala ya kuchaguliwa. Kesi nyingine ilifunguliwa mwaka 2006.
Kuanzia hapo, mahakama
ilipokea kesi tatu mwaka 2007, kesi moja mwaka 2008 na moja mwaka 2009 ambazo
zilisikilizwa na kuamuliwa. Mwaka 2010 mahakama ilipokea kesi tisa ambazo bado
zinasikilizwa, na mwaka huu, mahakama imepokea kesi tano.
Kesi zinazofunguliwa ni za
madai kama uchaguzi, gharama za kesi, unyanyasaji, fidia ya uchelewezaji wa
bidhaa kama bandarini, katiba na pensheni.
Swali: Miaka 10 ya uhai wa EACJ ni mingi, lakini kitu
cha ajabu bado haifahaki sana kwa wananchi,
unasemaje kuhusu hilo na kama
kuna mikakati yo yote ya makusudi kuifanya ifahamike zaidi?
Jibu: Hiyo
ni moja ya changamoto kwetu. Haifahamiki kiasi cha kutosha lakini tumedhamiria
kujitangaza sana.
Tunataka kuvitumia vyombo vya habari katika kuteleza matakwa hayo, kama vile televisheni, radio, magazeti na majarida.
Tutakuwa tunarekodi vipindi na kuvipeleka katika vituo vya televisheni au radio
kwa manufaa ya wananchi ili waweze kuifahamu mahakama yao na shughuli inazofanya.
Njia nyingine tunayoituma
kujitangaza kwa wananchi ni kufanya mikutano na
makongamano na tumekwishazungumza na wanasheria wote wa nchi tano husika
na kongamano la mwisho litafanyika Nairobi, Kenya, Juni 28 na 29 mwaka huu.
Mkakati mwingine wa
kuhakikisha kwamba mahakama hii inafahamika zaidi ni uamuzi wa kufanya vikao
vya mahakama kwa nchi wanachama. Hatua hii naona itasaidia kufanya watu waifahamu
zaidi mahakama yao.
Swali: Bajeti ya EACJ ni kiasi gani na inatosheleza
mahitaji?
Jibu: Bajeti
yetu ni dola za Marekani 2,280,000. Hazitoshelezi bali tunajikita katika
vipaumbele zaidi kama ilivyoanishwa katika
Mpango Mkakati wa 2010-2015.