MHADHIRI
mwandamizi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, Shule ya Dar es Salaam, Dk. Honest
Ngowi, ameitahadharisha serikali kujenga misingi mizuri ya kunufaika na
raslimali za madini na gesi kwa kujifunza kutoka nchi zingine za Afrika ambazo
raslimali hizo zimegeuka kuwa laana badala ya kujenga uchumi wa nchi zao na
wananchi kwa ujumla.
Akitoa
mifano ya nchi za Afrika (majina yanahifadhiwa) zenye madini, gesi na
mafuta, Dk. Ngowi alisema hakuna ambayo
imeonekana kunufaika na raslimali hizo,
huku wananchi wake wakiendelea kuogelea katika lindi la umaskini.
Dk. Ngowi alitoa tahadhari hiyo kufuatia
kugundulika kwa madini mengi ya uranium na gesi nchini, lakini akaonyesha
wasiwasi wake iwapo raslimali hizo kama
zimewekewa mfumo mzuri wa kunufaisha taifa na wananchi wake.
Alikuwa
akizungumza kwenye mafunzo ya siku moja yanayoandaliwa na Shirika la Hakikazi
Catalyst la jijini Arusha ya kuwajengea uwezo wananchi na viongozi wa kata,
vijiji na vitongoji kutoka mikoa ya Tanga, Kilimanjaro, Arusha na Manyara, kuhusu
kupanda kwa gharama za maisha na umaskini Tanzania: Serikali inafanya jitihada gani na wananchi
wanashiriki vipi?
“Bila kuweka
mfumo mzuri wa mkunufaisha mwananchi,
madini, gesi na baadaye mafuta, yatakuwa ni laana kwao…watakaonufaika
sio wananchi bali mataifa
yaliyoendelea,” alisema.
Alisema
baadhi ya nchi zenye kuzalisha mafuta mengi na mazuri duniani, hazijaendelea kiuchumi kutokana na kukosa
mfumo sahihi wa kunufaika na mafuta hayo.
Kuhusu
kupanda kwa bei ya mafuta, hususan, mikoani, Dk. Ngowi alipendekeza kujengwa
kwa bomba la mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza ili kuwarahisha
upatikanaji wake katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.
Hata hivyo,
mikakati ya ujenzi wa bomba hilo
ulianza tangu wakati wa awamu ya tatu ya Rais Ben Mkapa hadi miaka ya mwanzoni
ya awamu ya nne ya Rais Jakaya Kikwete, na mpaka sasa hakuna taarifa zo zote
zilizotolewa na serikali kuhusu kuendelea na ujenzi huo au la.