WAZIRI WA MAMBO YA NJE WA MALAWI, EPHRAIMU CHIUME
Mazungumzo ya mgogoro wa mpaka wa Ziwa Nyasa baina ya Serikali za Tanzania na Malawi ya kwama, huku Tanzania ikifanikiwa kuwashawishi Malawi kusitisha shughuli za utafiti wa mafuta katika kipindi chote cha kutafuta muafaka.
Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo uliongozwa na Waziri Membe na makatibu wakuu, Patrick Lutabanzibwa (Ardhi), John Haule (Mambo ya Nje) Waziri wa Ardhi, Prof. Anna Tibaijuka na Balozi wa Tanzania nchini Malawi, Patrick Tsere.
Akizungumza wakati wa kuhitimisha kikao cha usuluhishi kilichohusisha timu za wataalamu na viongozi wa wizara husika wa nchi hizo kilichomalizika Jumamosi Agosti 25 2012 usiku mjini Lilongwe, Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Bernard Membe, alisema Tanzania bado ina amini katika mazungumzo ili kufikia muafaka.
Alisema kuwa pamoja na sababu mbalimbali zilizotolewa na Malawi juu ya umiliki wa eneo lote la Ziwa Nyasa, msimamo wa Tanzania uko wazi kwa kuzingatia vielelezo vya historia vilivyoachwa na wakoloni na sheria za kimataifa kuhusu mpaka kuwa katikati ya ziwa hilo.
Membe alisema kuwa licha ya Serikali ya Malawi kuonesha kila dalili za kukwamisha mazungumzo hayo yaliyoanza kupitia vikao mbalimbali nchini humo, viongozi wa nchi hizo kupitia mkutano wa kutafuta suluhu uliomalizika juzi usiku wameamua kuunda timu za wataalamu.
“Licha ya kuwasilisha vielelezo kuonesha uhalali wa mpaka, hatukuweza kufikia muafaka, tumefika mahali pa kuhitaji msaada tuzitume tume za nchi zetu zitoe mapendekezo ya nini kifanyike, maana kuna kila dalili kwamba sisi wenyewe tutashindwa kuendelea zaidi,” alisema.
Alisema kuwa wataalamu kutoka Malawi na Tanzana watakutana Septemba jijini Dar es Salaam ili waweze kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuwapata wasuluhishi wa mgogoro huo pamoja na faida na hasara ya njia watakazozipendekeza.
Membe aliongeza kuwa, timu za wataalamu zitakazoundwa zitatoa mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa marais wa nchi hizo katika kuelekea hatua ya pili ya utatuzi wa mgogoro huo, ikiwemo kumtafuta msuluhishi au kwenda kwenye mahakama ya kimataifa.
Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Malawi, Ephraimu Chiume, alisisitiza kuwa licha ya mgogoro huo kuhitaji busara zaidi, bado serikali yake inaamini kuwa mpaka kati yake na Tanzania uko upande wa mashariki mwa Ziwa Nyasa na unatenganishwa na ardhi ya Tanzania.
Alisema kutokana na unyeti wa suala lenyewe na eneo hilo pamoja na historia ya nchi yake, anapenda kuona ufumbuzi ukipatikana haraka ili wananchi wa nchi mbili waweze kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
“Ni matumaini yangu mkutano wa Dar es Salaam utakaofanyika Septemba utazaa matunda ili suala hili lipatiwe ufumbuzi, na ikiwezekana tupate msaada wa sheria za kimataifa kwa sababu suala hili liko kisheria zaidi,” alisema Chiume.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia