Upande wa utetezi katika kesi
inayomkali mtuhumiwa ambaye bado anasakwa, Pheneas Munyarugarama
ameiomba Mahakama ya Rufaa ya taasisi inayorithi kazi za Mahakama za
Umoja wa Mataifa, MICT, tawi la Arusha,kubadili uamuzi wa kuipeleka kesi
ya mteja wao kusikilizwa nchini Rwanda kwa madai kuwa majaji wa nchi
hiyo hawatamtendea haki mtuhumiwa huyo.
Juni 28, 2012,Mahakama iliamuru kesi ya Munyarugarama,afisa wa zamani wa jeshi la Rwanda,ipelekwe kusikilizwa nchini humo.
Lakini katika maelezo ya rufaa, Wakili wa zamu wa mtuhumiwa huyo,
Francis Stolla wa Tanzania, alieleza kwamba majaji ambao ni raia wa
Rwanda, na pia kutokana na umri wao, walishuhudia uhalifu wa mauaji ya
kimbari ukitendeka,hivyo anadai hawawezi kutenda haki bila upendeleo
iwapo watasikiliza kesi za mauaji ya kimbari nchini Rwanda.
‘’Hali ya kuwepo uwezekano wa
majaji kupendelea upande mmoja wa kesi hauunganishwi na Mahakama za
Rwanda kama taasisi lakini unahusishwa na majaji binafsi.Upande wa
utetezi unaamini kwamba Mahakama za Rwanda zinaweza zikawa huru kama
taasisi lakini majaji wanaweza kuupendelea upande mmoja,’’ inasomeka
sehemu ya maombi hayo yaliyowasilishwa Julai 31, 2012.
Katika majibu ya hoja hizo Agosti 7, mwendesha mashitaka alitaka
maombi hayo ya upande wa utetezi yatupwe kwa sababu yamewasilishwa
yakiwa yamecheleweshwa tena bila kupata ruhusa kwanza kutoka mahakamani.
Umedai pia kwamba upande wa utetezi umeshindwa kuonyesha makosa
yaliyofanywa na mahakama ya awali kuonyesha kwamba majaji wa Rwanda
wangekuwa na upendeleo.
Mkuu wa Kitengo cha Rufaa na Ushauri wa Sheria, James Arguin alieleza
kwamba maombi ya rufaa ya Munyarugarama yaliletwa siku tano baada ya
kupita muda uliotakiwa kisheria Julai 26, 2012.
Alifafanua kwamba Wakili wa zamu wa mtuhumiwa anadai kwamba
amewasilisha maombi hayo kwa nia njema kutokana na matatizo ya kifamilia
ambayo hakuyatarajia.
Munyarugarama, ambaye alikuwa Kamanda wa kambi ya jeshi ya Gako,
wilaya ya Kanzenze,mkoa wa Kigali Vijijini kati ya mapema 1993 na Mei
1994, anashitakiwa kwa mauaji ya kimbari, kula njama za kufanya mauaji
hayo, uchochezi na uhalifu dhidi ya binadamu.