Baada ya kesi ya Butare yenye kuhusisha watu sita kusikilizwa kwa muda wa miaka 10 mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda (ICTR), kesi hiyo inaweza kuchukua muda mrefu pia kusikilizwa katika ngazi ya Mahakama ya Rufaa. Mwaka mmoja baada ya kutolewa kwa hukumu ya kesi hiyo, taratibu za kukata rufaa bado zinasuasua kutokana na matatizo ya kutafsiri hukumu hiyo toka lugha ya Kiingereza kwenda Kifaransa.
Juni 24, 2011, ICTR ilimhukumu Waziri wa zamani wa Wanawake na Masuala ya Familia wa Rwanda, Pauline Nyiramasuhuko, mtoto wake wa kiume, Arsen Shalom Ntahobali na meya wa zamani, Elie Ndayambaje vifungo vya maisha jela kwa kushiriki kwao katika mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994, katika mkoa wa Butare, uliopo Kusini mwa Rwanda. Meya mwingine, Joseph Kanyabashi alihukumiwa kifungo cha miaka 35 jela, huku wakuu wawili wa zamani wa mikoa, Sylvain Nsabimana akihukumiwa kutumikia miaka 25 na mwenzake Alphonse Nteziryayo akipewa miaka 30. Wote wamekata rufaa lakini bado wanasubiri tafsiri ya hukumu hiyo ambayo iko katika lugha ya Kiingereza iwe kwenye lugha ya Kifaransa.
Ingawaje baadhi ya watu katika timu zao za utetezi wanazungumza Kiingereza, lugha ya kufanyia kazi kwa watu wote hao sita waliotiwa hatiani ni Kifaransa. Juni 24, 2011 Jaji Kiongozi katika mahakama iliyosikiliza kesi hiyo, William Hussein Sekule wa Tanzania, alisoma muhtasari tu wa hukumu hiyo kwa Kiingereza. Hukumu kamili kwa Kiingereza ilisambazwa kwa wahusika wote katika kesi hiyo wiki tatu baadaye. Hukumu hiyo yenye kurasa 1,500 bado inawatoa jasho maafisa wa mahakama hii kuitafsiri kwenda lugha ya Kifaransa.
‘’Tunafanyakazi kwa bidii kubwa. Siyo jambo rahisi kutafsiri nyaraka zenye kujaa maneno lukuki ya kisheria ’’ alisema mmoja wa wafasiri ambaye aliomba kutotajwa jina lake. ‘’ Na katika masuala ya kisheria pengine kuzidi masuala mengine unatakiwa kuwa makini sana unapotafsiri. Tunatarajia kukamilisha kazi hiyo katika wiki chache zijazo.’’
Mtafsiri mmoja kutoka Cameroon, Francois Bembatoum aliliambia Shirika la Habari la Hirondelle Februari 2010 kwamba timu hiyo ambayo haionekani machoni pa watu lakini inafanyakazi ambayo ni lazima ifanyike, ilikuwa tayari imeanza kazi hiyo. ‘’Kutafsiri siyo sawa na kurudufu,’’ alisema. ‘’Vipo viwango vya kimataifa vinavyotambulika sawia katika kazi za kutafsiri. Hatuna budi kupata rasilimali watu ya kutosha kulingana na uzito wa kazi uliopo, vingenevyo, lazima itachukua muda mrefu.’’
Tangu wakati huo, kwa mujibu wa mfanyakazi mmoja wa idara ya Masijala, kitengo cha lugha hakikusalimika katika zoezi la kupunguzwa kwa taratibu wafanyakazi kadiri ICTR inavyokaribia kuhitimisha kazi zake ifikapo 2014.
Maandalizi ya awali
Mahakama ilizishauri timu za utetezi zenye watu wenye kujua lugha ya Kiingereza, kuanza kuandaa hati za awali za rufaa kwa kutumia hukumu ya Kiingereza, ambayo inaweza kufanyiwa marekebisho madogo pindi hukumu ya lugha ya Kifaransa itakapopatikana. Wakili wa Nsabimana, Josette Kadji anasema timu yake imekuwa ikifanya hivyo.’’Tumekuwa tukifanya kazi kwa kutumia hukumu ya Kiingereza, huku tukisubiri nakala ya Kifaransa. Tukiipata, tutakuwa na siku 60 za kukamilisha rufaa yetu kwa maandishi.’’
Kanyabashi anasubiri tafsiri ya nyaraka nyingine ikiwa ni pamoja na hiyo ya hukumu, kwa sababu mwendesha mashitaka ameamua kukata rufaa dhidi ya hukumu yake pekee. Pindi watu hao waliotiwa hatiani wakikamilisha kuwasilisha hoja zao kwa maandishi, mwendesha mashitaka naye atapewa muda wa kujibu hoja hizo. Na pale tu baada ya majaji kusoma nyaraka zote hizo, ndipo mahakama itakapopanga tarehe ya kusikiliza rufaa husika. ‘’Labda mwishoni mwa mwaka huu, au labda mwaka ujao,’’ anasema Kadji.