Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya
Jinai (ICC) Jumanne imetangaza utaratibu wa kuwalipa fidia waathirika wa
uhalifu uliomtia hatiani Thomas Lubanga huku Marekani ikirejea msimamo
wake wa kusaidia juhudi za kuwatia mbaroni watuhumiwa ambao bado
wanasakwa na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya Rwanda
(ICTR).
ICC
Majaji wapanga utaratibu wa kulipa fidia wathirika wa uhalifu wa
Lubanga: Jumanne wiki hii, majaji wa ICC wameamuru Mfuko wa Kulipa Fidia
wa Waathirkika wa Uhalifu uliomtia hatiani, Kiongozi wa waasi wa
Jamhuri ya Kimokrasia ya Congo (DRC), Thamas Lubanga kupanga utaratibu
wa namna ya kugawa fidia hiyo.Wamefafanua kwamba Mfuko huo hauna budi
kupeleka kundi la wataalam Ituru, Mashariki mwa DRC kulikofanyika
uhalifu huo ili kubaini jamii zilizoathiriwa na uhalifu wa Lubanga kati
ya Septemba 1, 2002 na Agosti 13, 2003. Lubanga alitiwa hatiani kwa
uhalifu wa kivita kwa kuwasajili watoto katika kundi lake la waasi
kupigana vita eneo la Ituri.Alihukumiwa kifungo cha miaka 14, jela.
Mahakama yasimamisha tarehe ya Libya kuwasilisha hoja kesi ya mtoto
wa Gaddafi: Mahakama inayosikiliza hoja za awali katika kesi ya Saif
Al-Islam, mtoto wa Kiongozi wa zamani wa Libya Muammar Gaddafi,
imesitisha maagizo yake ya kutaka serikali ya Libya kuwasilisha hoja
zake Agosti 13, kama ilivyoamriwa awali.Libya iliatakiwa kujibu hoja za
mwendesha mashiataka juu ya suala la kesi ya Saif Al-slama kusikilizwa
na ICC.Hata hivyo majaji pia hawakuweza kupanga tarehe nyingine ya
kusikiliza hoja hizo hadi watakapopata maendeleo ya kesi ya Saif mbele
ya mahakama za Libya na uteuzi kukamilika kwa uundwaji wa Wizara ya
Sheria ya nchi hiyo kufuatia uchaguzi uliofanywa hivi karibuni.
ICTR
Marekani yapania kusaka watuhumiwa
ambao hajakamatwa: Marekani imerudia msimamo wake wa kusaidia juhudi za
kuwasaka watuhumiwa tisa wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ambao bado
hawajatiwa mbaroni na Mahakama ya Kimataifa ya Mauaji ya Kimbari ya
Rwanda (ICTR).Msimamo huo umerejewa na Balozi wa Marekani
anayeshughulikia Uhalifu wa Kivita, Stephen Rapp Jumatatu, makao makuu
ya mahakama hiyo,mjini Arusha, Tanzania.
Mwendesha mashitaka ataka ombi la rufaa la utetezi litupwe: Mwendesha
mashitaka imeiomba mahakama kutupilia mbali ombi la upande wa utetezi
katika kesi inayomkabili mtuhumiwa ambaye bado anasakwa, Pheneas
Munyarugarama kutaka amri ya kesi ya mteja wake kwenda kusikilizwa
Rwanda ibatilishwe.Upande wa utetezi umeomba amri hiyo iliyotolewa Juni
28, 2012 ibatilishwe kwa madai kwamba majaji wa nchi hiyo watatoa
maamuzi ya upendeleo iwapo itasikilizwa nchini humo. Mwendesha mashitaka
alitaka maombi hayo ya upande wa utetezi yatupwe kwa sababu
yamewasilishwa yakiwa yamecheleweshwa tena bila kupata ruhusa kwanza
kutoka mahakamani.
RWANDA
Kesi ya Mugesera kuanza kusikilizwa Septemba 17: Mahakama Kuu nchini
Rwanda Alhamisi wiki hii ilitangaza kwamba kesi ya Leon Mugesera
anayeshitakliwa kwa mauaji ya kimbari itaanza kusikilizwa rasmi Septemba
17, mwaka huu. Mugesera aliyerejeshwa nchini humo kutoka Canada Januari
mwaka huu anashitakiwa kwa kuchochea mauaji ya kimbari kupitia hotuba
yake aliyoitoa kwa lugha ya Kinyarwanda mwaka 1992.
WIKI HII
Kesi ya Bemba kuendelea kusikilizwa wiki hii Kesi ya Kiongozi wa
zamani wa kundi la waasi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) la
MLC, Jean Pierre Bemba itaendelea kusikilizwa Jumanne ijayo, Agosti 14.
Bemba anashitakiwa kutokana na uhalifu uliofanywa na kundi lake katika
Jamhuri ya Afrika ya Kati kati ya mwaka 2002 na 2003. Upande wa utetezi
unatarajiwa kuanza kuleta mashahidi wake.