Mwendesha Mashiataka Mkuu wa Libya, Jumatano wiki hii ametangaza kuwa kesi ya mtoto wa kiongozi wa zamani wa nchi hiyo, Saif Al-Islam Gaddafi sasa itasikilizwa nchini humo huku siku hiyo pia Senegal ilitiliana saini na Umoja wa Afrika (AU) kuanzisha mahakama maalum ya kushughulikia kesi dhidi ya Rais wa zamani wa Chad, Hissene Habre.
LIBYA
Kesi ya mtoto wa Gaddafi kusikilizwa nchini Libya: Kesi ya Seif Al-Islam, mtoto wa kiume wa kiongozi wa zamani wa Libya, Muammar Gaddafi sasa itasikilizwa nchini humo Septemba mwaka huu. Kwa mujibu wa Msemaji wa Mwendesha Mashitaka wa Libya, kesi ya Seif Al-Islam (40) itasikilizwa katika mji wa Zintan ambako amekuwa akilishikiliwa kizuizini tangu alipotiwa mbaroni mwaka jana.Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC) iliyotoa hati ya kukamatwa kwa Seif kwa makosa ya uhalifu dhidi ya binadamu inasema kwamba inafahamu taarifa hiyo, lakini serikali ya Libya haijawasiliana nayo. Seif mwenyewe anataka ashitakiwe mbele ya mahakama ya ICC iliyopo The Hague, Uholanzi.Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanahofia kwamba Seif anaweza kukabiliwa na hukumu ya kifo iwapo kesi yake itasikilizwa nchini humo.
SENEGAL
Senegal na AU kuanzisha mahakama kumshitaki Habre: Senegal Jumatano wiki hii imetiliana saini makubaliano ya kuanzisha mahakama maalum, mahususi kwa ajili ya kushughulikia mashitaka dhidi ya kiongozi wa zamani wa Chad, Hissene Habre. Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) Julai 21, 2012 ilitoa uamuzi kwamba Senegal imekiuka wajibu wake wa kimataifa kwa kushindwa kufanya maandalizi ya awali juu ya taarifa muhimu zinazohusiana na uhalifu uliofanywa na kiongozi huyo.Uamuzi huo uliitaka nchi hiyo ‘’bila kuchelewa zaidi kuwasilisha kesi hiyo mbele ya mamlaka inayofaa ili ishughulikiwe.’’ Kiongozi huyo anakabiliwa na tuhuma za uhalifu wa kivita na mauaji lukuki ya wanasiasa wakati wa utawala wake kati ya 1982 na 1990.
Kesi ya Bemba yaahirishwa hadi Septemba 3. Mtaalamu wa Kijeshi, Jenerali mstaafu wa Ufaransa, Jacques Seara ambaye ni shahidi wa kwanza wa utetezi katika kesi inayomkabli Jean Pierre Bemba alihitimisha ushahidi wake Alhamisi. Kufuatia hatua hiyo kesi imeahirishwa hadi Septemba 3, 2012 ambapo upande wa utetezi unatarajiwa kuendelea kuita mashahidi wake.Bemba,Kamanda wa zamani wa kundi la waasi la MLC, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Makamu wa Rais wa zamani wa nchi hiyo, anashitakiwa kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita unaodaiwa kufanywa mwaka 2002-2003, katika Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
SCSL
Mawakili wa Taylor kumtumia Jaji Sow: Mawakili wa Charles Taylor wiki hii wametangaza nia yao ya kutaka kumwita kizimbani Jaji Malick Sow wakati wa usikilizaji wa awali wa rufaa ya kesi inayomkabili kiongozi huyo wa zamani wa Liberia.Jaji huyo raia wa Senegal alitimuliwa kazi Mei mwaka huu baada ya juhudi zake za kutoa maamuzi tofauti katika hukumu ya Taylor Aprili 26, 2012. Taylor alihukumiwa kifungo cha miaka 50 jela baada ya kutiwa hatiani kwa uhalifu dhidi ya binadamu na uhalifu wa kivita.
Post a Comment
unashauriwa kutoa maoni muda na wakati wowote na kama unahabari yeyote unaruhusiwa kututumia